RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameipongeza Kamati ya Madawati kwa Skuli za Serikali kwa kusimamia na kuhamasisha wahisani na wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi katika kuchangia utatuzi wa uhaba wa vikalio.

Rais Dk. Shein aliyasema hayo leo Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na baadae kukabidhiwa ripoti na Kamati ya Madawati ya Zanzibar ambayo inaongozwa na  Mwenyekiti wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora Haroun Ali Suleiman.

Rais Dk. Shein ameahidi kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Saba na ile ijayo itaendelea kuiitafutia ufumbuzi changamoto ya uhaba wa vikalio ili kuhakikisha wanafunzi wote wa Msingi na Sekondari kwa Unguja na Pemba hakuna anaekaa chini.

Aidha, Rais Dk. Shein alisema kuwa Kamati hiyo aliyoiunda mnamo tarehe 27 Julai mwaka 2016 imeweza kufanya kazi nzuri ya kusimamia na kuhamasisha wahisani na wafanyabiashara wa ndani na nje ya Nchi katika kuchangia utatuzi wa uhaba wa vikalio kwa skuli za Zanzibar.

‘”Serikali imefanya jitihada kubwa ya kuhakikisha inawapatia wanafunzi wa Skuli za Serikali madawati kwani hapo mwanzo wengi wao walikuwa hawana pa kukaa tumeanza na tumetimiza wajibu wetu”,alisema Rais Dk. Shein.

Mapema Mwenyekiti wa Kamati ya Madawati ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora Haroun Ali Suleiman alisema kuwa  kufuatia makusanyo ya fedha za Madawati TZS Bilioni 7.6 Kamati ilinunua vikalio kwa awamu mbili.

Alisema kuwa Awamu ya kwanza ilifanyika kwa vikalio vya wanafunzi wa Sekondari vilivyojumuisha seti 44,620 ya viti na meza na awamu ya pili ni kwa vikalio vya wanafunzi wa Skuli za Msingi vilivyojumuisha meza 11,560 za wanafunzi watatu watatu na  viti 34,680.