Rais wa Rwanda Paul Kagame ameelezea kuwa chimbuko la mgogoro baina ya nchi yake na nchi ya Uganda ni la tangu miaka 20 iliyopita nchi ya Uganda ikitaka kuangusha utawala wake.

Akihutubia mkutano wa kitaifa Rais Kagame amesema mgogoro huo ulishika kasi miaka ya hivi karibuni kutokana na Serikali ya Uganda kuunga mkono kundi la RNC linalopinga Rwanda.

Pia alisema kundi hilo  linatumiwa na Uganda kuwanyanyasa raia wake wanaotembelea au wanaoishi nchini Uganda.

Akihutubia mkutano wa kitaifa unaomkutanisha na viongozi wengine kuanzia ngazi ya mashinani, Rais  Kagame amezungumzia kwa kirefu mgogoro huo.

Akifafanua mgogoro huo Rais Kagame amerejelea kitabu kinachoitwa ‘From Genocied to continental War” ambacho kiliandikwa na Gerard Prunier mwandishi wa vitabu kutoka Ufaransa.

Rais Kagame amesema kwamba mwandishi huyo aliandika kwamba alikutana na waziri wa zamani wa mambo ya ndani marehemu Seth Sendashonga mwaka 1998 pamoja  na maofisa wakuu wa jeshi la Uganda na kuzungumzia mipango ya kumsaidia Sendashonga ili kuangusha utawala wa Kagame.

Mwandishi huyo katika kitabu chake kwa mujibu wa  maelezo ya Rais Kagame, Uganda ilikuwa imemuahidi kumsaidia kijeshi.

‘Sababu ya mimi kurejelea kuzungumza haya nimetaka kuwaonyesha mfululizo wa jinsi mambo yalivyokwenda mnamo miaka 20 iliyopita.

Tulijaribu kufanya mikutano ya hapa na pale ili kutafuta suluhu.lakini matatizo hayo hayaishi.Ukweli ni kwamba Seth Sendashonga alifariki dunia kwa kuwa alivuka mstari mwekundu.Sifurahii kusema hivyo lakini pia sijutii kifo chake” Seth Sendashonga aliuawa katika mazingira ya kutatanisha mwaka 1998 mjini Nairobi alipokuwa uhamishoni baada ya kutofautiana na utawala wa Rwanda.

Rais Kagame amesema mgogoro huo ulishika kasi hivi karibuni kufuatia  wananchi wa Rwanda wanaoingia nchini Uganda au kufanyia kazi nchini humo kushikwa na kuzuiliwa sehemu ambazo hazijulikani na kuteswa.