Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli amemteua Profesa Shukurani Elisha Manya kuwa Kamishna wa Madini ambaye atakuwa Mtendaji Mkuu wa Tume ya Madini nchini na kumfuta kazi Kamishna aliyekuwepo Mhandisi Benjamin Mchwampaka.

Rais amefanya uteuzi huo leo katika hafla ya kumuapisha Doto Mashaka Biteko kuwa Naibu Waziri wa Madini ambaye anaungana na Naibu Waziri Stanslaus Nyongo katika wizara hiyo, chini ya Waziri Angela Kairuki.

Rais Magufuli ameeleza kuwa amefanya uteuzi huo baada ya kupewa taarifa kuwa kuna tatizo katika utendaji wa kamisheni ya Madini.

“Nimeambiwa Kamishina wa Madini ni tatizo inawezekana yupo hapa, Nimeamua kumteua Prof. Shukrani Elisha Manya atakuwa Kamishina wa Madini na ndo atakuwa Mtendaji Mkuu wa Tume ya Madini.” Amesema Rais Dkt Magufuli.

Kamishna aliyekuwepo,  Mhandisi Benjamin Mchwampaka amehudumu katika nafasi hiyo kwa siku 263 tangu alipoteuliwa mpaka leo uteuzi wake ulipotenguliwa na Rais magufuli.

Aidha rais Magufuli amewataka watendaji wote wa Wizara ya Madini kuchapa kazi kwa bidii kwani mpaka sasa bado utendaji wao bado unasuasua.

“Wizara ya madini ina changamoto nyingi, na hata sasa hivi bado ina changamoto nyingi. Bado wizara ya madini haifanyi kazi vizuri sana. Nikizungumza kwa kupamba nitakuwa mnafiki,”amesema Rais Magufuli.