Rais Dkt. John Pombe Magufuli amemuagiza Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. John Jingu, kusimamia kwa karibu usajili na uratibu wa NGO nchini kwa kuwa kumekuwa na vitendo vya ovyo vinavyofanywa na asasi hizo.

Dk. Magufuli alisisitiza kuwa NGO zinatakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia sheria ambazo pamoja na mambo mengine zinatakiwa kuendesha shughuli zao kwa uwazi hususani katika masuala ya mapato na matumizi ya fedha za ufadhili wa shughuli zake.

“Nataka ukasimamie usajili na uratibu wa NGO, najua zipo chini ya maendeleo ya jamii, kasimamie kuwe na uwazi wa utendaji kazi wa NGO,” alisisitiza Rais Magufuli.

Rais Magufuli aliyasema hayo jana katika Ikulu ndogo ya Chamwino, wakati wa hafla ya kuwaapisha Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. John Njingu, Mkurugenzi wa Takukuru, Kamishna wa Polisi, Diwani Athumani na Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Balozi Dk. Azizi Malima.

Rais Magufuli pia alimtaka Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Diwani Athumani, kuongeza kasi ya kushughulikia tatizo la rushwa nchini kwa kuhakikisha wote wanaokabiliwa na tuhuma za kujihusisha na rushwa, wanafikishwa mahakamani na sheria inachukua mkondo wake.

Rais Magufuli pia alimtaka Diwani kuuangalia upya muundo wa Takukuru ili uweke bayana majukumu ya Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru.

Alimtaka kuhakikisha watendaji wa taasisi hiyo wanaoonekana kutofanya kazi kwa tija na kujihusisha na vitendo vya rushwa wanachukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kuondolewa kazini na kufikishwa mahakamani.

“Nataka ukaisafishe Takukuru, kuna baadhi ya wafanyakazi pale wanajihusisha na rushwa, kawaondoe, nataka kuona Takukuru inashughulikia rushwa kwelikweli hasa rushwa kubwakubwa, ukipita huko vijijini wananchi wanateseka sana, wananyanyaswa na kuna dhuluma nyingi sana na tatizo kubwa ni rushwa,” alisisitiza Rais Magufuli.

Viongozi walioapishwa na Rais Magufuli pia wamekula kiapo cha uadilifu kwa watumishi wa umma kilichoongozwa na Kamishna wa Maadili, Jaji mstaafu Harold Nsekela na baada ya viapo vyao walimshukuru Rais kwa kuwateua na wamemwahidi kufanya kazi kwa juhudi, maarifa na kwa kutanguliza maslahi ya taifa.

Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. John Jingu, alimhakikishia Rais Magufuli kutekeleza majukumu yake kwa akili, moyo na nguvu zake zote, ili kufikia mafanikio anayoyatarajiwa na yanayotarajiwa na Watanzania.

“Nikuahidi mheshimiwa Rais nitafanya kazi kwa nguvu na akili zangu zote kwa kushirikiana na wenzangu katika wizara ili kuhakikisha mafanikio yanapatikana,” alisema Dk. Jingu.

Hafla ya kuapishwa kwa viongozi hao imefanyika katika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwamo Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge, Job Ndugai, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, mawaziri, viongozi wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama na viongozi wa mkoa wa Dodoma wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo, Dk. Binilith Satano Mahenge.