Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohamed Mahmoud amesema hali ya ulinzi na usalama katika Mkoa wake iko vizuri kutokana na ushirikiano mkubwa anaoupata kutoka katika Vikosi vya ulinzi na Usalama nchini.

Ameyasema hayo Ofisini kwake Vuga alipokuwa akitoa maelezo kuhusu hali ya ulinzi na usalama ya Mkoa wake kwa Kamishna wa Uhamiaji Tanzania General Anna Pita Makakala. Kamishna Makakala yupo Zanzibar katika mwendelezo wa ziara yake katika Mkoa wa Mjini Magharibi.

Aidha Mkuu huyo amesema Mkoa wa Mjini Magharibi ni miongoni mwa Mikoa 31 ya Tanzania  ambayo ina wakaazi wengi kutokana na kuja kwa Wageni wanaotoka nje na ndani ya Afrika, hivyo kupelekea baadhi ya wageni hao kujihusisha na vitendo vya kihalifu ikiwemo wizi wa watoto.

Akizugumzia suala la Bandari bubu Mkuu huyo ameeleza kuwa zipo banadari bubu nyigi ambazo wageni na wenyeji huzitumia kama ni sehemu ya kupitishia biashara zao za kimagendo ikiwemo wanyama lakini wanajitahidi kudhibiti hali hiyo.

Amefahamisha kuwa wamekuwa wakishirikiana na Vikosi vya ulinzi, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini SUMATRA pamoja na Wananchi mbalimbali na kufunga Kamera za Usalama (CCTV Camera) katika maeneo muhimu ili kukabiliana na uhalifu Mkoni humo.

Katika kupambana na uhamiji haramu na kudhibiti hali hiyo amesema wanafanya Doria na msako katika maeneo tofauti ili kuufanya mkoa huo uendelee katika hali ya amani na utulivu.

Kwa upande wake Kamishna Makakala amezipongeza juhudi zinazofanywa na Mkuu huyo katika kupambana na matukio ya kiuhalifu.

Aidha Kamishna Makakala ameuomba uongozi wa Mkoa kuzidisha ushirikiano katika vyombo vya Ulinzi na Usalama ili kuimarisha usalama wa Mkoa na Taifa kwa ujumla.

Kamishna Makakala alikuwa na ziara ya siku mbili Kisiwani Unguja kutembelea maeneo mbalimbali ikiwa ni miongoni mwa juhudi zake za kuimarisha mashirikiano ya taasisi yake na taasisi nyingine kwa lengo la kuifanya Tanzania iendelee katika hali ya amani na utulivu.