Mwanamuziki Richard Martin Maarufu Rich Mavoko ambaye hivi karibuni aliwashtua mashabiki wake katika mitandao baada ya kujitabiria kifo, amefunguka zaidi sababu ya kufanya hivyo.


Richard Martin, amesema alichomaanisha katika ujumbe huo ni tofauti na watu walivyoelewa huku akieleza kuwa hawalaumu kwa kuwa imechangiwa na nchi kupatwa na misiba mfululizo.


Katika ukurasa wake kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram, Mavoko aliandika maneno mafupi yaliyoambatana na picha ikimuonyesha amejiinamia: ‘Ni siku ya mwisho ya maisha yangu yaliyobaki’.


Maneno yaliyoibua gumzo huku wengine wakimtakia apumzike kwa amani kwa kuandika maneno mafupi ya kingereza RIP.
Katika mahojiano na Mwananchi jana msanii huyo ambaye anatamba na wimbo ‘Wezele’ kwa sasa amesema katika ujumbe huo alioundika Machi 16 mwaka huu, alikuwa ana maanisha kuwa siku hiyo haitajirudia.

“Mfano leo ni siku ya Alhamisi (jana), ni wazi kwamba hakuna Alhamisi nyingine kama hii itakayojirudia ndicho nilichokuwa ninamaanisha wakati naandika ujumbe huo na mbona ni vitu vinaimbwa kwenye nyimbo mbalimbali, vinaandikwa kwenye vitabu labda kwa kuwa wengi wetu sio wapenzi wa kusoma.
“Lakini kwa wengine wanaojua kuchanganua mambo nina imani waliposoma neno kwa neno walinielewa nini nilimaanisha na hao wanaodhani labda nilikuwa nataka kufa, wapi niliaga kuwa nakufa?”