HMoja ya tatizo kubwa ulimwenguni ambalo limekuwa likipigiwa kelele na kuwekewa kila aina ya utaratibu wa kuling’oa kwa mbinu zote kutokana na athari zake kuwa ni kubwa ni rushwa.

Janga ambalo baadhi ya wakati hufikia hata baaadhi ya viongozi au watumishi kusimamishwa kazi na wengine kuchukuliwa maamuzi ya kufikishwa Mahakamani kutokana na kukiuka maadili ya kazi zao.

Zanzibar ikiwa ni sehemu ya duniani nayo imekua ikiathirika  kutokana na vitendo vya kutoa na kupokea  rushwa ambavyo baadhi ya wakati vinaelezwa kuwa ni sehemu ya kurudisha nyuma uchumi wa nchi.

Hasa kwa kuwa hakuna nchi yoyote duniani inayofikisha huduma bora kwa wananchi wake ikiwamo maji safi na salama, miundombinu bora, huduma ya nishati, elimu, afya, ujenzi wa miji mipya pamoja na mambo mengine bila ya kuwa na uchumi imara.

Ni wazi kwamba kutokana na hali hiyo ndio maana Zanzibar nayo imeonekana kupania vya kutosha katika kuhakikisha mapambano dhidi ya rusha yanafanikiwa ili kuona maenedeleo endelevu yanapatikana kwa wananchi wote.

Miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na uazishwaji wa Mamlaka ya Rushuwa na uhujumu wa Uchumi Zanzibar (Zaeca) ambayo ina kazi kubwa ya kuhakikisha inakabiliana na vitendo hivyo.

Licha ya kuwepo kwa baadhi ya mafanikio baada ya kuanzishwa kwa Mamlaka hiyo ikiwamo kuchukuliwa hatua baadhi ya watumishi wa umma baada ya kubainika kuhusika na vitendo vya rushwa na uhujumu wa uchumi.

kuna maeneo yanahitaji kuangaliwa zaidi ili kufikia dhana ya mapambano haya miongonia mwa mambo hayo ni:-

Changamoto za kisheria

Licha ya Zaeca kufanya juhudi mbali mbali katika mapambano dhidi ya rushwa, lakini ukosefu wa sheria ya kumlinda shahidi wa matukio au tukio la rushwa kunachangia kwa baadhi ya mashahidi kutokuwa tayari kutoa ushahidi pindi wakihitajika kutoa ushahidi.

Naibu Mrajisi wa Mahakama kuu ya Zanzibar, Salum Hassan amesema ni wazi kwamba ukosefu wa sheria hiyo hupelekea kwa baadhi ya mashahidi kushindwa kutoa taarifa za matukio hayo hata kama wanazifahamu, hiyo ni kutokana na mtu binafsi kuangalia usalama wake kwanza.

Amesema kutokana na hali hiyo ndio maana baadhi ya kesi za matukio ya rushwa huchukua muda mrefu kumaliza na nyengine kufutwa kutokana na ukosefu wa ushahidi, ijapokuwa mtuhumiwa alitenda kosa husika.

Amesema licha ya kuwepo kwa sheria ya Kuizuia rushwa na uhujumu wa uchumi Zanzibar ya mwaka 2012, ambayo baadhi ya vifungu vyake vya sheria vinaonesha shahidi inawezekana asitajwe katika uendeshaji wa kesi, kitendo ambacho bado kinawapa wakati mgumu wananchi kutoa ushahidi katika matukio ya rushwa na uhujumu wa uchumi.

Amesema hali hiyo hutokana na vifungu hivyo bado havijaweka wazi jinsi gani shahidi anaweza kulindwa katika maisha yake pindi ikitokea dalili za hatari kutokana na ushahidi wake huo.

Salum amesema ili kuwe na kinga bora inayoonesha shahidi anakuwa na kinga kuanzia mwanzo wa ushahidi, wakati wa kesi Mahakamani hata baada ya kumaliza kesi, hakuna budi ni kuanzishwa sheria maalum ya ‘ kinga dhidi ya shahidi wa rushwa na uhujumu wa uchumi’ ambayo itakuwa na nguvu hata katika uendeshaji kesi za aina hizo Mahakamani.

Ameendelea kusema mbali ya sheria hiyo lakini pia kitendo cha kesi za Rushwa kusikilizwa katika Mahaka kuu nacho kinachangia kurudisha nyuma mapambano hayo.

Alitoan ushari kwa kusema ni vyema kwa Mahakama za Wilaya anzo zikawa na uwezo wa kusikiliza na kutoa maamuzi ya kesi hizo ili kuona malengo ya mapambao ya rushwa yanafikia.

Mkuu wa uendeshaji Mahakama kuu na Mahakama ya rufaa Tanzania kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar, Suleiman Haji Hassan amesema ni wazi kwamba kuwepo kwa sheria maalum ya kumlinda shahidi wa kesi za aina hiyo ni moja ya mambo ya msingi.

Amesema pindi kukiwa na sheria hiyo kuna matukio mengi yanayohusiana na vitendo vya rushwa au uhujumu wa uchumi yanweza kuibuka, kutokana na wananchi  kujenga imani ya kuwa salama kutokana na kinga watakayoipata kupitia sheria hiyo.

Amesema licha ya jitihada za Zaeca juu ya kukabiliana na vitendo vya rushwa inahitajika kuweka mikakati madhubuti juu ya mapambano hayo ikiwamo  kuhakikisha  kunakuwa na wataalam wazalendo waliobobea katika masuala ya rushwa na uhujumu wa uchumi.

Alipendekeza kwa wafanyakazi wa Zaeca kupelekwa katika nchi zilizoendeleo  kujifunza namana ya kuendesha mapambano dhidi ya rushwa ili kuongeza ujuzi wao.

Mwanasheria dhamana Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Pemba, Ali Rajab Ali amesema kama sheria inatamka makosa yote yaanzie mahakama kuu, hapo utekelezaji wake unakua wa kusuasua, akidai kwamba ni lazima kufanyike kwa maboresho ya sheria hiyo ya Zaeca.

Alisema ni wazi kwamba sheria ya Zaeca inahitaji maboresho kutokana na inavyosema kwamba hata mtu akikamatwa kwa kosa la shilingi 100, alazimika kupelekwa Mahakama kuu jambo ambalo ni vigumu sana na huchangia kudorora kwa uendeshaji wa haraka wa kesi za rushwa.

Kuporomoka maadili

Kuporomoka kwa maadili na kukosekana uadilifu  kwa baadhi ya wananchi pamoja na baadhi ya watenda wa umma ni miongoni mwa sababu zinazochangia kuwepo vitendo vya rushwa na uhujumu wa uchumi nchini.

Makundi hayo mara nyingi hutawaliwa na tamaa ya nafsi hasa katika utoaji wa huduma za kijamii mfano huduma ya afya, elimu, ajira pamoja na huduma nyengine.

Mmoja wa waliowahi kukumbwa na tukio la kuombwa rushwa ambaye hakutaka kutaja jina lake alisema aliwahi kutoa zaidi ya shiling million moja kwa ajili ya kupatiwa ajira lakini hadi hii leo hakuna kazi aliyoipata.

Hata hivyo baadhi ya watumishi wa serikali wameshuhudiwa wakipokea rushwa ili waweze kutoa huduma kwa wananchi ambazo walitakiwa kupewa  bila ya malipo yoyote.

Mfano wa hayo Zaeca iliwahi kumnasa Eid  Salum Wakilambe  ambaye anaadaiwa kuwa ni Diwani  kwa tuhuma za rushwa, ambapo.

Afisa Uhusiano wa Mamlaka hiyo Mwanaidi Suleiman amesema Diwani huyo amekamatwa kwa tuhuma za kuomba rushwa ya  shiling 150,000 kutoka kwa  mwananchi wa wadi hiyo ya Muembe majogoo ili ampatie kibali  cha kuendelea na ujenzi.

Lakini  pia Zaeca imeshawahi kukamata Askari Polisi pamoja na baadhi  ya watumishi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ambao wanadaiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa na uhujumu wa uchumi.

Shekh Mohamed Kassi kutoka Wakfu na Mali ya Amana amesema kukosekana maadili kwa jamii kunasababishwa na ushukaji wa imani ya dini, hivyo alitoa rai kwa wanajamii kurudi katika vitabu vyao vya dini ili kurejesha imani zinatazowadumisha kufanya uadilifu kwa kila jambo.

Katibu Tume ya maadili ya viongozi wa umma, Kubingwa Mashaka Simba amesema licha ya tume yao kutoa elimu lakini  ili kufanikisha hali hiyo hakuna budi kwa Mashekeh, Mapadri, viongozi wa siasa, wazazi pamoja na viongozi wengine  kutumia nafasi zao  vyema kwa kuwa wa kwanza kuelimisha wanajamii juu ya athari za rushwa.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar (ZAECA), Mussa Haji Ali amesema katika kufanikisha mapamabano ya rushwa wamekuwa wakaifanya mikutano mbali mbali ili kuona jamii inapata elimu juu ya athari za rushwa.

Kwa upande wa Katibu wa Ofisi ya Mufti, Sheikh Fadhil Soraga amesema ni muhimu watendaji pamoja na taasisi mbali mbali  kuungana kwa pamoja katika kujikita katika mapambano dhidi ya vitendo hivyo.

Udhibiti maeneo ya mapato

Licha ya serikali kuweka utaratibu wa ukusanyaji kodi, lengo ni kuona mapato hayo yanatumika katika kuleta maendeleo nchini, lakini bado kuna baadhi ya wafanyabiashara na watumishi wa umma wanaonekana kukwamisha jitihada hizo kwa maslahi yao.

Mfano ni utolewaji wa huduma kwa baadhi ya taasisi unaweza kulipia huduma bila ya kupewa risiti, lakini wakati mwengine unaweza kupewa risiti bila ya hiyo risiti kuandikwa kiasi ulicholipia huduma.

Mtaalam wa uchumi kutoka kitengo cha uchumi Zanzibar, Said Haji Mrisho alitoa mfano mwengine kwa kusema kwamba mfano mfanyabishara katoa makontena zaidi ya kumi lakini katika risiti ya utoaji huandikwa makontena matatu tu, huku wengine wakitumia njia za magendo kwa ajili ya kuuza au kusafirisha bidhaa.

Mrisho amesema vitendo hivyo vyote ni uwepo wa mianya ya kodi, ambapo baadhi ya wakati serikali haifikii malengo ya ukusanyaji wa mapato na ndipo huchukuliwa maamuzi ya kuongezwa kodi kwa baadhi ya bidhaa.

Amesema kupanda kwa kodi hakuwaathiri wafanyabishara tu, bali kuwaathiri zaidi wananchi hasa wa kipato cha chini kutokana na upandaji wa kodi husababisha kupanda harama za maisha.

Amesema serikali hupanga mipango mingi ya maendeleo kutokana na malengo yake ya ukusanyaji kodi, hivyo ikitokea mfanyabishara au mtumishi wa umma kujihusisha na vitendo hivyo huisababishia serikali kutofikisha huduma bora kwa jamii kama ilivyotajia.

Kupanda kwa gharama za maisha

Mtaalam wa uchumi kutoka kitengo cha uchumi Zanzibar, Said Haji Mrisho alisema kitendo cha kupanda kwa gharama za maisha nacho baadhi ya wakati huwafanya watumishi wa umma kujiingiza katika vitendo hivyo ili kukidhi mahitaji yao.

Amesema ni vyema kwa serikali kuhakikisha inadhibiti mianya yote ya kupanda kwa bei za bidhaa ambazo hudaiwa kuwa ni chanzo cha kutokea kwa vitendo vya rushwa na uhujumu wa uchumi Zanzibar.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman, amesema Zanzibar ni miongoni mwa nchi zinazoathiriwa na tatizo la rushwa duniani hivyo ni vyema kila mmoja akawa balozi wa mapambano ya rushwa ili kuona maendeleo ya nchi yanaimarika.