Hoja za mara kwa marakutoka katika baraza na maskani mbalimbali na hata kwenye baraza za wasusiambapo mara nyingi jamii yetu hutumia maeneo hayo kujadili masuala mbalimbaliya kijamii, kiuchumi na Nyanja nyenginezo wakiwa huru bila kuwepo itifaki zozote.Huko hoja zao kuhusiana na rushwa zimegawika kama ifuatavyo:

Hoja ya Kwanza

Hoja ya kwanza huwa inawazungumzia askari wa usalama barabarani (Trafiki) mbao ndio kundi linalolaumiwa zaidi katika vitendo vya rushwa. Hoja kuhusiana na Trafiki ni kama ifuatavyo:- Trafiki hawawezi kuacha kuchukua rushwa kwasababu ya kuwa na mishahara kidogo, wanashirikiana na wakubwa wao na wakipeleka kesi mahakamani hawapati kitu.

Hoja ya Pili

Hoja hii inaelekezwa zaidi kwenye huduma za Afya hususani Hospitali na vituo vya Afya. Hoja za wanajamii ni kwamba Hospitali wanapokea rushwa kwasababu ya udogo wa mishahara, ni rahisi kumshawishi mgonjwa na watu wake kutoa rushwa kutokana na shida ya mgonjwa  hivyo ni lazima wakubali kutoa rushwa, na wakati mwengine mgonjwa na watu wake hutengeneza mazingira ya kutoa rushwa ili wapate huduma.

Hoja ya Tatu

Hoja hii kutoka katikamitaa yetu imejikita zaidi kuzungumzia kadhia ya rushwa ya ngono ambayowanaitaja kuwepo katika maeneo ya kazi na taasisi za elimu kama skuli na vyuo. Hojakubwa kutoka mitaani ni kwamba rushwa ya ngono inatolewa kwasababu mtafutajikazi anakuwa anahitaji kazi na hujirahisisha kwa makusudi ili aweze kupatakupitia vitendo hivyo visivyokubalika na vyenye kuleta ukakasi. Hali kadhalikakwa mwenye dhamana ya kutoa kazi nae hutengeneza mazingira yanayopelekeakutokea kwa vitendi vya rushwa.

Kila eneo na kila aina ya rushwa  ambayo imetajwa na zinatajwazinasababu na hoja zake, kwetu sisi hizi zote si sababu za msingi na ni hojazisizo na mashiko na ni kung’ang’ania utamaduni na tabia zisizokuwa maridhawa.

Nitakupa mfano mmoja ambao ulitokezea hapa hapa visiwani petu Zanzibar. Kuna rafiki yangu mmoja alitoka Dar es Salaam kuja Zanzibar kwa ajili ya masomo, siku moja akapita kwenye mkahawa mmoja maarufu pale Malindi, mjini Unguja kupata Chai. Wakati anaendelea kunywa Chai alitokea mtu mmoja wa makamo anahema kwa nguvu;  Yule mzee wa makamo alisogea mbio kwa muuzaji wa Chai na kumwambia alisahau kumlipa pesa yake na kwamba alikua kashafika Darajani ndipo akakumbuka na kurudi mbio kumletea muuzaji fedha zake. Akamaliza kwa kusema anaogopa sana dhulma.

Yule rafiki yangu akashangaa kwa tabia na utamaduni ule. Kwake yeye lilikua jambo la ajabu sana na akajisemea kimoyomoyo ‘Huyu mzee mshamba sana, kapata zali la mentali lakini mshamba’.

Nimeutoa mfano huo kuonyesha utamaduni na tabia zetu katika masuala ya kununua, kuuza, kuokota kitu cha mtu; sote tunafahamu kuwa hapa petu anaezidishiwa pesa wakati wa kununua huzirejesha, anaeokota hupeleka Studio Rahaleo kutangaziwa.

Kwanini rushwa haturejeshi au hatupeleki pale studio Rahaleo, badala yake tunadai kwamba mishahara midogo, tunahitaji uharaka hatutaki kuzungushwa na tunahalalisha hayo kwa msemo penye udhia penyeza rupia.

Inawezekana, Tubadili Utamaduni , Tubadili Tabia.

Cha kufanya ni kuhakikisha elimu juu ya ubaya wa rushwa inatolewa kuanzia kwenye ngazi ya familia na ielezwe kuwa rushwa haiongezi mshahara wala haisaidii kupata kitu badala yake inaharibu kila kitu. Kwenye familia ndipo walipo madaktari, askari polisi, mahakimu, wapima viwanja, wasimamizi wa masoko, Rais, Sheha, mwakilishi, mbunge na mpiga kura kwa kuwataja kwa uchache kabisa.

Tubadili Utamaduni naTabia kwenye rushwa ili Uchumi wetu ukue kwani asilimia kumi (10%) haitokuwepo,viongozi wa ngazi mbalimbali hawatopokea rushwa ya aina yoyote ikiwemo zile zamikataba ya miradi mbalimbali na matokeo yake mshahara utaongezeka na kilahuduma itapatikana bila urasimu.

Tulianza na baraza, maskani na kwa msusi tumalizie huko huko kwa kusema imetosha sasa kulalamika kuhusu kadhia za rushwa na sasa tubadili utamaduni na tabia kuhusiana na rushwa na asiyebadilika tumfyekelee mbali kwa kumfikisha kwa kiboko wa rushwa ZAECA.