Rushwa ya ngono UDSM yachukuwa sura mpya, TGNP yatoa neno

MTANDAO wa Jinsia Tanzania (TGNP Mtandao) umekemea rushwa ya ngono katika jamii na kusema Tanzania haitaweza kufikia maendeleo ya viwanda au uchumi wa kati wenye manufaa kwa watu kama hakutakuwa na juhudi za kupiga vita ukatili wa kijinsia na hasa rushwa ya ngono.

MKURUGENZI WA TGNP MTANDAO, LILIAN LIUNDI, PICHA NA MTANDAO

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, katika maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia, Mkurugenzi wa TGNP Mtandao, Lilian Liundi, alisema tatizo la rushwa ya ngono kwa jamii linarudisha nyuma maendeleo, utu wa mwanamke na kupunguza morali ya kufanya kazi.

“Kwa mujibu wa Chama cha Wanawake Majaji Tanzania (TAWJA), moja ya changamoto inayowasumbua wanawake wa Tanzania wanapotafuta ajira ni kuombwa rushwa ya ngono. Hii imerudisha maendeleo nyuma na kuwakosesha haki yao ya msingi ya kupata ajira au huduma ya msingi,” alisema Lilian.

Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Vicensia Shule, kuibua tuhuma za rushwa ya ngono katika chuo hicho, akidai changamoto ya wahadhiri kuomba rushwa ya ngono kwa wanafunzi imekithiri chuoni hapo.

Akizungumza katika kongomano hilo la kupinga ukatili wa kijinsia, Lilian, alisema matarajio ya ndoto ya wanawake zinakatizwa na watu wachache ambao ni hatarishi, hivyo jamii inapaswa kufanya kazi ya ziada kuhakikisha inatokomeza kabisa rushwa ya ngono kwa kuwahimiza wasichana na wanawake wote kuvunja ukimya.

“Waathirika wengi katika jamii ni kinamama, ndugu, watoto, mabinti zetu, au watumishi wenzetu katika maeneo ya kazi ambao wakati mwingine hushia kufariki mapema baada ya kuambukizwa virusi vya Ukimwi,” alisema Lilian.

Aliwataka washiriki wa kongamano hilo kuungana na wanaharakati wengine wa haki za wanawake na usawa wa kijinsia kupinga vikali vitendo hivyo, kwa kuwa rushwa ya ngono ni kinyume na Sheria ya Takukuru ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007.

Sheria hiyo inatamka wazi kuwa mtu yeyote anayeombwa rushwa ya ngono ili apate huduma au haki yake, anapaswa kutoa taarifa Takukuru au vyombo vingine vya dola kuhakikisha mhusika anakamatwa na kuchukuliwa hatua.

Tanzania imeridhia mikataba mingi pamoja na matamko yanayolenga kuleta usawa wa jinsia na kutoa fursa kwa wanawake na kuwalinda dhidi ya dhuluma na aina yoyote ya ukatili na udhalilishaji.

Mikataba hiyo ni pamoja na Dira ya Taifa, Mkataba wa Kupinga Dhuluma na Ukatili dhidi ya Wanawake, Azimio la Beijing na Mpango Kazi, Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), Mkataba wa SADC wa usawa wa kijinsia na ule wa nyongeza kuhusu utokomezaji wa dhuluma na ubaguzi dhidi ya wanawake na watoto (CRC) na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano.

Lilian alisema pamoja na kuwapo katiba ya nchi inayoainisha haki sawa kati ya wanawake na wanaume, bado usawa huo haujafikiwa katika kuhakikisha wanawake wanajengewa uwezo wa kisheria na kupata haki zao.

Alisisitiza umuhimu wa kuboresha mazingira ya ajira na uhusiano kati ya mwajiri na mwajiriwa, ili kutokomeza ukatili wa kijinsia sehemu za kazi na kuongeza uzalishaji wenye tija kwa maendeleo endelevu, kukuza na kulinda utu wa mwanamke kwa kutokomeza ukatili wa kijnsia na kuongeza ujasiri kwa wanawake, kukuza maendeleo ya kiuchumi na kuongeza nguvu katika ongezeko la Tanzania ya viwanda na kutokomeza rushwa ya ngono ili kumpa mwanamke heshima eneo la kazi.