Mhubiri na mmiliki wa kituo cha redio cha Amazing Grace, raia wa Marekani Gregg Schoof aliyekamatwa mapema wiki hii jijini Kigali, amefukuzwa nchini Ruwanda.

Schoof amekuwa Nchini Rwanda tangu mwaka 2003, kuhubiri lakini mwaka uliopita kituo chake che redio kilifungwa baada ya kuhubiri kupitia kituo hicho kuwa, wanawake ni ‘malaya na ibilisi.’

Alikamatwa siku ya Jumatatu, akiwa na mwanaye wakati alipokuwa anataka kuwahutubia wanahabari jijini Kigali akidaiwa kutaka kuishtumu serikali ya Rwanda.

Idara ya uhamiaji inasema, mtoto wake aliachiliwa huru, lakini yeye amefukuzwa kwa sababu, kwanza kibali chake cha kufanya kazi kimeisha na hakuwa na sababu ya kuwa Rwanda maana kituo chake cha redio kilishafungwa.

Kanisa la Mhubiri huyo ni miongoni mwa Makanisa 700 yaliyofungwa mwezi Februari, baada ya kushindwa kutimiza masharti ya Serikali kuhusu kufungua Kanisa .