Waziri wa zamani wa Fedha nchini Pakistan amesema kuwa uamuzi wa hivi karibuni wa Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hautafikia natija yoyote.

Salman Shah ameyasema hayo katika mahojiano na Shirika la Habari la IRNA mjini Islamabad, mji mkuu wa Pakistan kuhusiana na hatua ya Washington ya kutorefusha kibali cha ununuzi wa mafuta ya Iran na kusisitiza kwamba hatua hiyo haina faida. Aidha amesema kwamba Washington inatakiwa kutenganisha ulimwengu wa siasa na biashara.

Waziri wa Fedha na Uchumi wa zamani wa Pakistan ameongeza kwamba, vikwazo vya mafuta vya Marekani dhidi ya Iran havina faida kwa upande wowote na kwamba Washington haifai kuwafanya wahanga wafanyabiashara wa mafuta. Salman Shah amebainisha kwamba uamuzi wa Marekani wa kutorefusha muda wa kibali cha ununuzi wa mafuta ya Iran utaifanya hali ya mambo kuwa mbaya .

kwa kuvuruga uthabiti wa soko la mafuta duniani. Inafaa kuashiria kuwa uamuzi huo wa Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran umeendelea kupingwa vikali na wateja wa mafuta ya nchi hii hususan China, Korea Kusini, India, Japan na Uturuki.