Utamaduni (culture)  ni nyenzo muhimu katika maisha ya mwanaadamu na hata taifa kwa ujumla, kwani ndio unaompangia vipi aishi.

Wataalamu tokea zama na tangu waliwahi kutuambia kuwa asilimia 99 ya wakaazi wa Zanzibar ni waisilamu, hivyo bila ya shaka tokea zama hizo waliishi katika misingi ya dini hiyo pamoja na zile mila za kizanzibari walizokubaliana.

Nikitaja asilimia hiyo kwa  wazanzibari isifahamike vibaya kuwa hakuna waumini wa dini nyengine, wapo na ni wazaliwa haswa wa visiwa hivi.

Makala hii hailengi kuelezea udini, bali inakusudia kueleza umuhimu wa utamaduni pamoja na athari zake hasa pale watu wanapoanza kuweka pembeni utamaduni wao na kufuata kwengine kunapowadanganya kuwa kunawafaa.

Katika kuutunza utamamduni wa Mzanzibari , serikali imekua ikifanya jitihada kubwa kuhakikisha utamaduni haupotei wala kubadilika lengo ni kuonesha kuwa utamaduni ni nyenzo muhimu katika maisha.

Dhana ya Utamaduni ni dhana pana, ni mfumo mzima wa maisha ambao wananchi wanaishi kupitia mila , silka na desturi hizo, miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na ndoa ambapo ndani yake   kunapatikana kitu kiitwacho  “SINGO”.

Nimegusia ndoa kwakua katika mila na tamaduni za kizanzibari ili ufanye tendo la JIMAI ni lazima utangaze ndoa, ukamilishe masharti yote   ukabidhiwe  mke na ndipo unapokua huru kwa tendo hilo, kinyume chake hata uwe na watoto 100 na wake unaowajua wewe ikiwa umewapata nje ya ndoa hilo ni kosa tena la kisheria  kwa wazanzibari, maana utamaduni wa Mzanzibari unakwenda sambamba maadili ya Uisilamu.

Ingawa serikali inajidhatiti katika jitihada za kuhifadhi utamaduni huo lakini bado kuna baadhi ya taasisi zinarejesha nyuma juhudi hizo na kwa mwendo kasi zinavuruga tamaduni tofauti  na athari zake zimeshaanza kujitokeza .

Taasisi hizo zipo nyingi lakini leo nitazungumzia moja tu kati ya hizo kutokana na uchunguzi  niliyoanza kuufanya masiku kadhaa  yaliyo nyuma.

Nchini Zanzibar  kumejitokeza Saluni za kiume ndani yake kuna wafanyakazi wakike   wanaoshughulika na ufanyaji wa singo (scrub) pamoja na masaji (kukanda mwili) na wanaofanyiwa ni wateja wakiume wanaofika kupata huduma.

Saluni hizi  zinapatikana kwa wingi ndani ya Mkoa wa Mjini Maghribi Unguja,  mkoa mama katika nchi hii ingawa kule Pemba pia zimeshaanza kuingia.

Inasemekana kuwa saluni hizi kwa kiwango kikubwa zinaharibu utamaduni wa mzanzibari, ni kwasababu, kwanza ni kinyume na tamaduni , mila na silka za mzanzibari,  mwanaume kusingwa na kukandwa kimahaba anastahili kufanyiwa na mkewe tu, na mwanamke afanyiwe na mumewe, iweje leo tamaduni hizi zikanyagwe na kufinyangwa kisha watu wabakie kimya !

Mengi  yaliyojificha katika saluni hizi  nitakujuulisha ili kujua kunanini ndani yake, au ile dhana iliyonifanya kufuatilia jambo hili si ya kweli, nikaamua kulivalia njuga na mengi niliyagundua.

Nilikwenda katika saluni moja kwa mchina Mombasa njia ya kuelekea Mpendae, kulikua na wanawake wasiopungua watatu (3) mmoja kati yao nilimuuliza.

Sista mambo vipi?

Poa tu mzima ?

Mzima sijui wewe?

Nami mzima

Ok poa, kuna huduma ya kufanya scrub (singo ) hapa ?

Ndio ipo, karibu ndani.

Alinichukua moja kwa moja hadi katika chumba chake maalum, ndani ya chumba hicho tulikua watu wawili tu (mimi na yeye).

Nimetangulia kusema ni chumba chake kwa sababu kulikua na vyumba tofauti na kila mfanyakazi inaonekana anachumba chake kwa mujibu wa mazingira yalivyokua.

Akanitaka kuketi katika kiti, baadae akanishika kichwa na kunilaza taratibu, kisha alinifungua vifungo vya fulana, baadae akaja na maji ya uvuguvugu na kitambaa na kuanza kunipangusa.

Mikono yake ilifika hadi chini ya shingo na kunipapasa kifua kwa hanjifu nyepesi na laini, hayo ni maandalizi tu ya kufanyiwa singo .

“Geuka kidogo tazama juu” aliniambia mwanamke huyo, sikua mkaidi.

Alianza kunipaka (mafuta ya kusugulia) na kuanza kunisinga, “unajisikiaje  na huu unaotoka ni uchafu utatakata vizuri tu,”aliniambia mrembo huyo.

Ilikua ni mazingira magumu sana kwangu lakini kwakua nimeamua kuchunguza ukweli juu ya utamaduni unavyoharibiwa nilijikaza kiume kwakua wananchi wanataka kuufahamu ukweli katika mambo yaliyojificha.

Niliamua kupenyeza maneno matamu ili kuhakikisha mbali na hili kuna lipi jengine?

“yaani leo najisikia raha sana kama nipo peponi, mtoto utaniuwa mie” akajibu “haha… kawaida tu mbona”

“samahani naweza kupata kampani yako leo usiku alau nijisikie mwenye bahati, maana nataka kukufaidi mtoto” alijibu “wewe tu mimi mbona sina tatizo”.

Alinisinga vizuri baadae akanikosha tena kwa maji ya uvuguvugu kisha akaniingiza chumbani kumaliza tuliyoyazungumza.

“Niambie sasa , kwani wewe unataka vipi” aliniuliza binti huyo

Nikamjibu “kama nitakupata usiku wote wa leo itakua vizuri mana inaonekana upo vizuri sana katika mambo yetu” akajibu “ok sawa kwangu hakunashida, utanilipa shilingi 70,000 na kama kukupunguzia tufanye  shilingi 60,000 tu”

Tulikubaliana hivyo, na hapo nikagundua ,  mbali na singo zinazofanyika lakini kuna uwezekano mkubwa wa kufanyika biashara ya ngono (ukahaba)

Nasema hivi kwa sabau, kama utakumbana na huduma hii na jinsi walivyo wajuzi katika kazi ni lazima tu utamsifia hapo hapo au ndio utaomba kwenda kumalizana kwa jinsi anavyofanya ujuzi wake katika kazi ( kwa sauti na vitendo)

Kwa lengo lilelile la kujiridhisha nilikwenda katika saluni nyengine (njia ya kuelekea Amani Mwanakwerekwe mkabala na car wash) nako pia nilihitaji huduma ya singo ambayo ni shilingi 3,000 karibu ya saluni zote.

Na nikaongeza huduma , sasa nikahitaji na masaji (kukandwa mwili) hii ni shilingi 30,000

Alikuja mwanamke mzuri aliyetimia, kama kawaida aliniweka katika kiti na kuanza kunipangusa, huyu alimzidi wa awali, alikichukua kichwa changu na kukiweka chini ya kifua chake na juu ya tumbo (katikati)  huku  akinipangusa.

Hali ilikua ngumu sana pia nilivumilia hadi akamaliza kazi yake, baadae aliniita chumbani kama kawaida kwa lengo la kunifanyia masaji.

“vua nguo nianze kukufanyia” alisema mwanamke huyo, aliashiria niwe mtupu zaidi ya pensi au nguo ya ndani kama ninayo.

Ukweli nilishindwa , nilijibabaisha kiume nionekane nimeghairi , ingawa hakuonyesha kuridhika huku akinilaumu kwamba nimeshamkosesha pesa.

Pia nilitaka kujiridhisha kwa mara nyengine tena juu ya biashara ambayo nina wasiwasi huwenda ikawa inafanyika chinichini (ukahaba wa mtu mmoja mmoja).

Nilimuuliza “hivi nikitaka nikuchukue ili ukanifanyie masaji kwangu itakuaje?” alijibu “ tatizo nipokazini , kama siku nakua frii hakunashida labda jaribu mwengine unayemuona anakuvutia”

Alimaanisha nijaribu mwengine humo humo katika wasichana wanaofanyakazi.

Kauli hii inaashiria nini ? ni kwamba ukimuona anaekuridhi katika dada hao unaweza kuzungumza nae na kuondokanae inategemea vipi munavyokubaliana, na sitaki nizame kukuelezea biashara hii , mada yetu ni utamaduni wa singo na kukandana.

Hii ndio hali kwa saluni karibu zote unazoziona kisiwani Unguja, maadili ya kizanzibari yamekua yakipotea siku hadi siku, tangu lini mwanaume kufanyiwa singo na asiyekua mkewe,

Bila ya shaka kupitia matendo hayo kunazaliwa athari nyingi miongoni mwa hizo ni huko kurahisika tendo la ngono kuwa ni kitu cha kawaida.

Kwakuwa wateje wengi wa huduma hizi ni vijana ingawa wamakamo na wazee wamo niliamua kuchukua mawazo yao juu ya uwepo wa saluni hizi na nilikutana na kijana wa miaka 25 hadi 27 (jina linahifadhiwa) alisema, saluni hizo zinaharibu utamaduni wa nchini.

Kwani kisheria kuna watu maalumu wanaopaswa kukusugua “pia hata biashara ya ukahaba inafanyika,  wakati anakufanyia scrub (singo) hapohapo munapatana kisha mutajuana munakutana wapi” alisema kijana huyo.

Mwananchi mwengine (dereva wa daladalaya K/samaki) alisema “kuna uwezekano mkubwa wa kufanya ngono, siku moja nilikwenda kupata huduma, hee! mwanamke kaniinamishia maziwa chini yangu huku ananitega , yaani ni mimi tu mwenyewe kutamka”alisema mwananchi huyo.

Akielezea  kwa hamasa aliniambia “maadili wanayaharibu kwetu hakuna vitu hivi” mwisho wa kunukuu.

Nilipowauliza ni kwanini wanakwenda katika saluni hizo, wengi walijibu kuwa, ni saluni za kawaida na hakuna ubaya kuingia hasa kwa kunyoa nywele.

Sheikh Khamis Bin Gharib kutoka Afisi ya Mufti Zanzibr nilipomgusia suala hili alisema, dini imekuja kukataza mambo yote yanayoshawishi kufanya zinaaa pale ALLAH S.W aliposema katika qur an ‘’wala musiikaribie zinaa’’

“kila jambo  linaloweza kumshawishi mtu kufanya zinaa  jambo hilo ni haramu, ikiwamo mas-ala ya saluni ambayo mtu akienda anafanyiwa masaji na mwanawake ambae si halali yake, yote ni haramu na nikuikaribisha zinaa”alisema Sheikh Khamis

Akiendelea kufafanua zaidi alisema, kugusa kumekatazwa, kutazama kwa makusudi kumekatazwa ,alisema jambo lolote linaloweza kuamsha hisia za mtu kufanya haramu jambo hilo limekatazwa katika dini ya kiisilamu.

Kwa upande wake Dk Omar Abdalla Adam Katibu Mtendaji, baraza la Sanaa na Utamaduni Zanzibar alisema , Zanzibar ina mila, silka, na desturi zake pia watu wanaheshimiana.

“mwanaume na mwanamke wanafanyia masaji ndani, hilo jambo halikubaliki na si sahihi wala si katika utamaduni wa Zanzibar” alisema katibu huyo.

Alisema masaluni hayo yapo na kuna baadhi ya vijana hawaridhiki lazima waende katika saluni hizo, hivyo hao wenyewe ndio wanaosababisha kuwepo kwa matendo hayo.

Akizungumzia msimamo wa serikali katika jambo hilo alisema serikali haikatazi uwepo wa  saluni , lakini kama kuna matendo ambayo yapo kinyume na utamaduni, hayo hayakubakili.

“wanaofanyiwa hivyo si watoto , ni watu wazima, kila mmoja ajione kuwa yeye ni mzanzibar na heshima zake, serikali itatoa taaluma kwa wananchi na kama kuna mtu anataka kusingwa amwambie mkewe au kufuata utaratibu mwengine” alisema katibu huyo.

Mmoja kati ya  wahusika wa utoawaji wa Leseni za biashara za saluni kutoka Baraza la Manispaa Mjini Zanzibar(jina limehifadhiwa) alisema “sipingi,  kuna uwezekano mkubwa wa kufanyika biashara ya ukahaba, huwa tunayaona, pia maadili yanavurugwa sana  maana kivazi tu cha mwanamke kinasema mimi nipo tayari kwa kila kitu” alisema afisa huyo

Alisema kawaida wanakua na utaratibu maalum wa kuzikagua saluni na nyengine kuzifungia kabisa ikibainika kuwa hawajalipia kodi lakini hawana utaratibu wa kutazama maadili ingawa mazingira yanaonyesha kuwa tamaduni zinaharibiwa.

“ masuala haya nilishayaripoti ingawa sio rasmi, lakini kwa jinsi unavyonieleza nitayaripoti rasmi na kuyatilia mkazo ili kuhakikisha maadili yanazingatiwa katika utoaji wa leseni kwa saluni hizi” alisema

 

Mwisho kabisa alisema, endapo kutapitishwa utarabu wa kuzungatia maadili katika utolewaji wa leseni hawatosita kuifungia saluni yoyote pale itakapoonekana kukiuka sheria hiyo.

Uchunguzi uliyofanywa na mwandishi wa makala hii umegundua kuwa, iwapo serikali haitolivalia njuga kwa nguvu zote suala hili , utamaduni wa mzanzibari unaweza kupotea haraka sana ikabaki kuwa kumbukumbu.

Kama kweli tunathamini utamaduni wetu kila mmoja awe mchunga kwa mwenzake kuhusu jambo hili, saluni hizi naziweka katika orodha ya majanga makubwa yanayoifika nchi ndogo ya Zanzibar, tulipo toka sipo tunapokwenda, lazima tuwe macho tutamalizika.

Na  Mwandishi wetu , Zanzibar.