Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu Serikali itatoa tamko la hatua iliyofikiwa katika kuwasaili madaktari watakaokwenda nchini Kenya kufanya kazi wakati wowote kuanzia leo.

Waziri Ummy Mwalimu aliyasema hayo katika mahojiano maalumu mjini hapa kuwa mchakato huo ungefikia asilimia 100 jana kukamilika kwake.

“Kimsingi hapa tunachokifanya ni kufanya majumuisho tu ya mchakato mzima ili sasa nitoe tamko la ni madaktari wangapi na wenye sifa zipi wamepatikana ili kwenda Kenya kutoa huduma za afya. “Nadhani hadi jioni leo (jana) kazi hii itakuwa imekamilika na hivyo naamini kesho tutatoa tamko letu rasmi juu ya mchakato huu mzima,” alisema.

Aitha amesema, Tanzania ilikubali ombi la kuipatia Kenya madaktari 500 watakaoisaidia nchi hiyo kukabiliana na tatizo la uhaba wa madaktari katika vituo vyake vya tiba hasa baada ya kutokea kwa mgomo wa madaktari nchini humo hivi karibuni.

Rais John Magufuli alikubali kutoa madaktari hao Machi 18, mwaka huu Ikulu jijini Dar es Salaam, baada ya kufanya mazungumzo na ujumbe wa viongozi wa Wizara ya Afya ya Kenya uliotumwa na Rais wa nchi hiyo, Uhuru Kenyatta.