Serikali imewarejesha kazini watumishi walioondolewa kwenye mfumo wa malipo ya mshahara kwa kukosa sifa ya cheti cha kufaulu mtihani wa elimu ya kidato cha nne.

Kauli ya Serikali imetolewa bungeni leo Aprili 9, 2018 na waziri wa nchi, ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala bora), George Mkuchika.

Serikali imesema watumishi wote wenye ajira za kudumu au ajira za mikataba (kwa watendaji wa vijiji na mitaa), au ajira za muda waliokuwa kazini kabla ya Mei 20, 2004 ulipoanza kutumika waraka wa utumishi namba moja wa mwaka 2004, warejeshwe kazini mara moja.

Mkuchika amesema Serikali imeagiza watumishi hao walipwe mishahara yao kwa kipindi chote ambacho walikuwa wameondolewa kazini na waendelee na ajira zao hadi watakapostaafu kwa mujibu wa sheria.

Hata hivyo, Mkuchika amesema Serikali haitawarudisha kazini watumishi waliothibitika kughushi vyeti vya kidato cha nne na kwamba, waliowapa ajira watachukuliwa hatua.

Mkuchika amesema uamuzi huo umefikiwa baada ya Serikali kupokea mapendekezo na malalamiko kutoka vyama vya wafanyakazi na kwa watumishi hao.

Sakata la Serikali kuwaondoa kazini watumishi wenye elimu ya darasa la saba wiki iliyopita lilizua mjadala bungeni, baada ya baadhi ya wabunge kutaka warejeshwe kazini.

Wakizungumza katika mjadala wa bajeti ya ofisi ya waziri mkuu kwa mwaka 2018/19, wabunge hao walisema watumishi hao hawakutendewa haki, huku mbunge wa Geita Mjini, Joseph Musukuma akisema hata yeye ana elimu ya darasa la saba lakini ni mwakilishi wa wananchi bungeni.