Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga aabainisha kuwa Serikali ipo katika hatua ya mwisho kuruhusu bucha za wanyamapori nchini na kutoa siku 30 kwa Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (Tawiri) kuwasilisha taarifa ya kitaalamu ya utekelezaji wa mpango huo.

Alibainisha hayo wakati alipozungumza na wafanyakazi wa Tawiri ijapokuwa watafiti mbalimbali wa taasisi hiyo, walionyesha wasiwasi kuhusu uanzishwaji wa bucha hizo nchini.

Mkurugenzi Mkuu wa Tawiri, Dk. Simon Mduma, alisema mpango huo unakuja bila kuwa na maandalizi ya kutosha kwa kuwa kunahitajika usimamizi wa hali ya juu.

Alitoa mfano wa nchi kama Afrika Kusini ambayo nyama ya wanyamapori inayouzwa kwa ajili ya kitoweo hupatikana katika mashamba maalumu yaliyoanzishwa na watu binafsi na siyo katika mapori maalumu ama katika mbuga za taifa.

Naibu Waziri Hasunga alitoa muda usiozidi mwezi mmoja kwa taasisi hiyo kuwasilisha taarifa ya kitaalamu kuhusiana na uanzishaji wa bucha hizo, huku akiwaeleza kuwa mpango huo upo katika hatua ya mwisho.

Aidha, katika hatua nyingine Hasunga aliiagiza Tawiri kuhakikisha inajiimarisha katika kufanya utafiti ili nchi ijitosheleze kwa takwimu za kutosha na za uhakika za wanyamapori tofauti na ilivyo sasa.

“Ni ukweli unaofahamika kwamba takwimu za wanyamapori nchini hazijakaa vizuri, mfano tumekuwa tukitafuta idadi ya tembo, simba au hata fisi, tunashindwa kuzipata na zikipatikana zinakuwa nusunusu,” alisisitiza Hasunga.

Katika taarifa ya Tawiri iliyotolewa na Mkurugenzi wake, Dk. Mduma ilibainisha jumla miradi ya tafiti kubwa 11 na zingine 10 ndogo zinaendelea kufanyika zikihusisha magonjwa, idadi, chanjo na kufuatilia mwenendo.

Baadhi ya miradi ya tafiti hizo ni pamoja na kufuatilia migongano baina ya watu na tembo katika maeneo ya Hifadhi za Serengeti na Mikumi, kutathmini uharibifu wa mazao na mienendo ya tembo waharibifu na maeneo wanayopendelea na kushauri njia ya kupunguza uharibifu huo.

Dk. Mduma alitaja utafiti mwingine ni wa ugonjwa wa bonde la ufa kwa watu, mifugo na wanyamapori katika mfumo wa kiikolojia wa Serengeti na wanachunguza kama kwenye panya na mbu kuna virusi vya ugonjwa huo ambao hujificha wakati hakuna mlipuko wa ugonjwa.

Alitaja utafiti mwingine ni wa chanjo ya ugonjwa wa homa ya nyumbu unaofanyika Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, ukilenga kuwakinga ng’ombe dhidi ya ugonjwa huo ambao umekuwa ukiwalazimu wafugaji kuhamisha mifugo na kuipeleka mbali kukwepa nyumbu wanaozaa ili mifugo yao isiambukizwe.

Alisema taasisi yake pia inasimamia na kuongoza mpango wa kuhifadhi vyura wa pekee katika Bonde la Kihansi na zaidi ya vyura 3,000 wameshapandikizwa katika maeneo yao ya asili baada ya kukuzwa na kuongezwa idadi katika maabara maalumu nchini Marekani.

Dk. Mduma alisema pia wanaendelea na mradi wa kupata idadi, mtawanyiko na mwenendo wa wanyamapori katika maeneo yaliyohifadhiwa na tayari wamekamilisha sensa katika mfumo wa ikolojia wa Serengeti pamoja na nyumbu wanaohama na sasa wanaendelea katika mfumo wa ikolojia wa Selous na Mikumi na sensa ya mamba.