Serikali yaanzisha Mjadala kuhusu kisima cha gesi Mtwara

Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani ameahidi kuchukuliwa kwa hatua za haraka za kudhibiti athari za mmomonyoko wa ardhi katika kisima cha gesi asilia, kilichopo kijiji cha Msimbati kwenye kisiwa cha Mnazi Bay mkoani kwa kujengea ukuta, kutokana na kuongezeka kwa kina cha bahari katika eneo hilo.

Aliyasema hayo jana baada ya kutembelea kisima hicho kwa lengo la kujionea na kujiridhisha athari ya mmomonyoko huo. Alisema, wakati wowote kisima hicho kinaweza kujaa maji ya bahari na kusababisha nchi kukosa nishati hiyo, hivyo ni vyema wataalamu wakaangalia namna ya kujenga ukuta ili kunusuru athari hiyo isitokee.

Alizitaka mamlaka zinazohusika na usimamizi wa kisima hicho, kukutana mara moja na kuweka mbinu za kuanza kujenga ukuta huo. “Ujio wangu hapa leo ni katika kuhakikisha kuwa kisima hiki kinabakia kuwa salama ili kuiwezesha nchi kuendelea kupata nishati itokanayo na gesi asilia”

Alisema madhara yaliishia umbali wa mita 150 kutoka eneo la bahari hadi kwenye kisima hicho, lakini sasa upo uwezekano wa madhara kufika jirani zaidi. Alisema, mwaka 2017 pia athari hiyo iliwahi kutokea, lakini haikuleta athari yoyote. Lakini, mwaka huu ni vema hatua za haraka zichukuliwe, kabla ya kutokea kwa madhara yaliyoanza kujitokeza.

“Anzeni sasa kufanya utaratibu wa kujenga ukuta kwa sababu mtafika mahala mtakosa hata mahali pa kuweka ukuta, kwani maji yakishafika huku haitawezekana kufanya chochote”alieleza