SERIKALI  imesikitishwa na vifo vya wanafunzi wanne ambao ni wasichana wa kidato cha nne kutoka shule ya sekondari Kimbiji iliyopo Kigamboni jijini Dar es salaam waliofariki kwa ajali ya maji walipokuwa wakiogelea katika bahari ya Hindi.

Vifo vya wanafunzi hao vilitokana na sherehe iliyoratibiwa na shule husika ili kuwapongeza wanafunzi hao wa kidato cha nne baada ya kufanya vyema mitihani yao ya kujipima.

Akizungumza kwa majonzi shuleni hapo,Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Selemani Jafo amesema serikali imepokea kwa masikitiko vifo hivyo na kutoa pole kwa wanafunzi, wazazi, na walimu wa shule hiyo kwa msiba huo mzito.

Waziri Jafo amewataka walimu wote nchini kujiepusha na ufanyaji wa sherehe za wanafunzi katika mazingira hatarishi. Aidha, Waziri Jafo aliwasilisha rambirambi kwa familia nne za wafiwa.

Wanafunzi waliofariki dunia ni Secilia Ernest Paulo, Selestina Vitus Malipesa, Agnetha Philipo Mlaki na Queen Leonard Mandala.