Serikali yataja sababu ya kufa kwa viwanda Zanzibar, yaahidi kuvifufua upya

Wajumbe wa baraza la Wawakilishi  wameiomba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar  iwaruhusu wawekezaji wandani na nje ya nchi  kuanzisha viwanda ili kuwapatia wananchi ajira pamoja na kuongeza pato la nchi.

Akijibu swali lililoulizwa na Mwakilishi wa Jimbo la Mfenesini Machana Othman Said Naibu Waziri wa Biashara na Viwanda Hassan Khamis Hafidh amesema Serikali ipo kwenye mpango Wa kuvifufua viwanda  vilivyokufa na kuwapa wawekezaji kuekeza kwenye maeneo hayo ili kuweza kuzalisha bidhaa kwalengo la kuleta maendeleo.

Amesema zipo sababu nyingi zilizosababisha kufa kwa viwanda vilivyokuwepo hapo awali Zanzibar hivyo kwasasa Serikali imejipanga kuhakikisha ujio wa viwanda vipya na kukabiliana na changamoto zote zilizopelekea kufa kwa viwanda vya mwanzo.

Mapema akizitaja sababu hizo ni kukosekana umeme wa uhakika, usumbufu wa huduma za meli kutokana na kasoro za bandari na ufinyu wa biashara Zanzibar,Ugumu wa kupata maeneo muwafaka kwa ajili ya viwanda  na ukosefu wa miundombinu katika maeneo huru pamoja na tija kwa  vijana walioajiriwa katika miradi.

Hata hivyo Hassan amesema mchakato wa kurejesha maeneo yaliyotajwa Serikalini unaendelea kwa kuanzia  kiwanda cha Cotex hivyo Wizara ya Biashara na Viwanda,Wizara ya Ardhi,Nyumba,Maji na Nishati pamoja na Wizara ya Fedha na Mipango walikaa pamoja kwa ajili ya kufanya tathmini  ya kiwanda hicho.

Amina Omar