Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Khadija Nassir, ameitaka Serikali kuanzisha Programu za Uzazi wa Mpango kwa wanaume kwa kuwa tafiti mbalimbali zinaonesha wana uwezo wa kuwapa mimba wanawake tisa kwa siku moja

Mbunge huyo alisema, tafiti mbalimbali Duniani zinaonesha kwamba mwanaume mmoja ana uwezo wa kuwapa mimba wanawake tisa kwa siku moja, wakati mwanamke mmoja ana uwezo wa kushika mimba moja kwa miezi tisa

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile, alisema ni dhana potofu kwamba Uzazi wa Mpango ni wanawake peke yao. Suala la Uzazi wa Mpango linawahusu wanaume vilevile na Serikali inahamasisha kinababa na mama kushiriki kwenye Uzazi wa Mpango Salama

Katika swali la msingi, Mbunge wa Viti Maalum (CHADEMA), Zubeda Sakuru alihoji, Serikali ina mkakati gani wa kuwawezesha Wakunga wa Jadi ili kupunguza vifo vya mama na mtoto hasa maeneo ya Vijijini?

Dkt. Ndugulile alijibu kuwa, Wizara inawatambua Wakunga wa Jadi kama watu muhimu katika Jamii, hivyo Wizara kwa kutambua umaarufu wao katika Jamii, inawatumia kufanya uhamasishaji wa wajawazito kujifungulia katika Vituo vya Kutolea Huduma na ikibidi kuwasindikiza