Kutokana na kushuka kwa bei za bidhaa za mafuta katika soko la dunia, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA) imetangaza bei mpya ya mafuta iliyoanza kutumika jana.

Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano (ZURA), Khuzaimat Bakari Kheri alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari, ofisini kwake Maisara.

Alisema, sababu za mabadiliko ya bei za mafuta ni kushuka kwa bei ya bidhaa hizo katika soko la dunia na gharama za usafirishaji na bima.

Alisema bei ya mafuta ya petroli kwa mwezi Juni ilikuwa ni shilingi 2,376 na sasa yatauzwa kwa shilingi 2,338 kwa lita.

“Mafuta ya dizeli yameshuka kwa asilimia 0.42 ambapo bei ya mwezi Juni ilikuwa ni shilingi 2,329 na bei ya mwezi Julai ni shilingi 2,319 ambayo ni tofauti ya shilingi 10,” alisema.

Kwa upande wa  mafuta ya taa, bei ya mwezi Juni ilikuwa shilingi 1,766 na sasa yatauzwa kwa shilingi  1,753 ambapo ni tofauti ya shilingi 13.

Alisema mafuta ya meli (banka) yatauzwa kwa shilingi 2,145 badala ya shilingi  2,155 ya mwezi Juni.

“Zura inapenda kuwajulisha wananchi kuwa, bei zilizotangazwa ndio halali zitakazoanza kutumika kuanzia jana,” alisema.