Watu wenye uwezo wametakiwa kuunga mkono juhudi za serikali katika kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu ili watoto hao waweze kunufaika na haki zao za msingi ikiwemo kupatiwa elimu na Matibabu.

Akijibu swali katika kikao cha Baraza la Wawakilishi Chukwani nje kidogo ya mji wa Zanzibar, Naibu Waziri wa Uwezeshaji ,Wazee ,Vijana ,Wanawake na watoto Shadya Muhammed Suleiman amesema kuna wimbi kubwa la watoto wanaohitaji msaada kutokana na familia zao kuwa masikini.

Amesema mpaka sasa Serikali inawatambua watoto Ishirini na mbili elfu mia moja na 43 kutoka shehia mbalimbali ikiwemo shehia ya Jangombe ,Kidongo chekundu, Magomeni, Nyerere na muembe Makumbi.

Aidha amesema licha ya Serikali kuwatambua watoto hao lakini wapo wengine bado hawajatambulika jambo linalopelekea kukosa haki zao za msingi zinazotolewa na miradi mbali mbali ya maendeleo ya kusaidia watoto.

Naibu Shadiya amewaomba Viongozi wa jimbo kuwa na utamaduni wa kutenga Bajeti maalumu kupitia fedha za Mfuko wa jimbo ili ziweze kutumika kwa ajili ya kuzisaidia kaya zinazoisha katika mazingira magumu kwa kuziwezesha kiuchumi ili kuwakwamua watoto na hali duni inayopelekea kukosa haki zao. 

Na;Fat-hiya Shehe Zanzibar24.