Shughuli za uokoaji zaendelea, Matumaini ya kuwapata manusura MV Nyerere yapotea

Shughuli za uokoaji baada ya kivuko cha MV Nyerere kuzama jana zinaendelea leo asubuhi, baada ya kusitishwa Alhamisi, kutokana na changamoto mbalimbali zikiwemo giza.

Zaidi ya watu 40 wamefariki huku wengine 37 wakiokolewa. Inakadiriwa kwamba wakati wa kuzama kwa kivuko hicho, kivuko hicho kilikuwa na zaidi ya abiria 100.

Kwa mujibu wa maafisa wa serikali eneo la Ukerewe, mpaka sasa chanzo cha ajali hiyo hakijafahamika huku nahodha wa meli hiyo akiwa miongoni mwa waliofariki dunia.

Mwandishi wa BBC David Nkya awali alizungumza na mkuu wa wilaya ya Ukerewe Kanali Lucas Maghembe ambaye anasema kufikia wakati wa kusitishwa kwa juhudi za uokoaji Alhamisi jioni, waokoaji walikuwa wamechunguza ndani ya kivuko hicho na hakukuwa na dalili za kuwapata manusura wakiwa hai.

Amesema uchunguzi unaendelea na iwapo kulikuwa na utepetevu fulani uliosababisha ajali hiyo wahusika watachukuliwa hatua za kinidhamu.

Kanali Magembe amesema pia kwamba ikizingatiwa kwamba maeneo mengi eneo hilo ni maji, mfano Ukerewe ambapo maji ni asilimia 90, eneo hilo linahitaji meli na vyombo vingine vya usafiri ambavyo vipo katika hali nzuri.