Simba SC inatarajiwa kucheza mchezo wa kirafiki na Sevilla utakaopigwa Mei 23 mwaka huu. Sevilla inayoshiriki Ligi Kuu nchini Hispania inaletwa nchini mwaka huu kwa udhamini wa kampuni ya Sportpesa.

Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao amesema awali walipokea wazo kutoka Sportpesa la kuzikutanisha timu za Simba na Yanga kisha bingwa ndio acheze na Sevilla, lakini ratiba ilikuwa inabana hivyo na kufanya uamuzi mengine.

“Wote tunajua kabisa kwamba Ligi yetu na ratiba yake jinsi hatukutaka kuharibu kalenda yetu, kwahiyo tulikaa vikao vingi sana na watu wa Sportpesa kujua tunafanyeje ili kuweza kupata timu ya kucheza mchezo huu, tuliandikiwa barua ya kuangalia namna ambavyo tunaweza kupata timu kwa kuangalia vigezo muhimu” ameeleza.

Aliongeza mechi hiyo sio bonanza kwani ni mechi ya ushindani kama ushindani wa mechi zingine ambazo zinakuwa zinafanyika.

Wakati kwa upande wa Sportpesa, Mkurugenzi wa utafiti, Udhibiti na Utawala, Abas Tarimba alisema katika uchaguzi wa timu waliumiza vichwa wakishirikiana na TFF mpaka kuja kupata timu hiyo.