Simba yafanya maajabu mbele ya Rais Magufuli

Moja ya matukio makubwa kwenye soka kwa mwaka 2018 ni lile la Rais John Magufuli kukubali kwa mara ya kwanza kushiriki kwenye tukio la michezo ambalo lilikuwa ni kukabidhi ubingwa wa ligi kuu soka Tanzania bara kwa mabingwa wa 2017/18, Simba SC.

Kwa upande wa Simba ni ngumu kusahau tukio hilo kutokana na mambo yaliyotokea siku hiyo ya Mei 17 mwaka huu ambapo Simba walikuwa wamecheza mechi 28 bila kufungwa lakini wakaharibiwa rekodi yao na Kagera Sugar kwa kufungwa bao 1-0.

Mbele ya mgeni rasmi Rais Magufuli, Simba walipokea kichapo hicho huku wakiwa tayari wamechukua ubingwa kwa kuwa na alama 68 ambazo zilikuwa hazifikiwa na Azam FC waliokuwa nafasi ya pili na alama 52 au Yanga waliokuwa katika nafasi ya 3 na alama 48.

Kitu kingine ambacho Simba haiwezi kukisahau siku hiyo kutoka kwa Rais ni hotuba yake baada ya mchezo huo kabla hajawakabidhi kombe lao ambapo alisisitiza mabadiliko katika kikosi chao vinginevyo hawawezi kufika mbali.

”Nimewaheshimu nimekuja hapa kuwapa kombe, basi huu usiwe mwisho wenu nawaomba mkabadilishe mchezo, ila kwa mpira niliouona leo hamuwezi kuchukua kombe la Afrika, ni lazima tubadilike kwa mpira huu hatuwezi”, alisema Rais Magufuli.

Kwasasa Simba ipo katika hatua ya makundi ya klabu bingwa Afrika ambapo wamepangwa kundi D na timu za Al Ahly ya Misri, JS Saoura ya Algeria na Vita Club ya DR Congo.