Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Skuli ya Sekondari ya Tumbatu Makame Khamis Nyange amezitaka Taasisi za Serikali na Binafsi kujitolea katika kuwapa elimu ya ziada Wanafunzi wa Skuli hiyo ili kuwajengea uwezo wanafunzi wanapomaliza masomo yao.

Akizungumza na Wanafunzi pamoja na Watendaji wa Bodi ya Mapato Zanzibar ZRB katika ukumbi wa Ofisi ya Wilaya ndogo ya Tumbatu, waliofika kisiwani hapo kwa ajili ya kutoa elimu ya kulipa kodi kwa Wanafunzi amesema Mwanafunzi anahitaji Elimu ya Skuli na ya kijamii ili kuweza kuwa raia mwema baada ya kumaliza Elimu ya Sekondari.

Amesema wakati umefika kwa Tasisi za Serikali kufuata Utaratibu wa ZRB katika kutoa elimu ya kwa wanafunzi wa Mikoa yote ya Zanzibar ili waweze kujua wajibu wao wanapomaliza elimu yao ya Sekondari.

Kwa Upande wake Afisa Uhusiano wa Bodi ya Mapato Zanzibar ZRB Makame Khamis Muhammed amesema lengo la kutoa elimu katika Kisiwa hicho ni muendelezo wa Utaratibu wao wa kutoa elimu ya mlipa kodi kwa wananchi wote wa Zanzibar.

Amesema Wanafunzi ni Wawakilishi wazuri kwa Familia hivyo wakipatiwa elimu hiyo wataweza kuisaidia serikali kufikia malengo waliyo yakusudia katika kutoa huduma bora kwa jamii pamoja na kuiwezesha Miradi ya Serikali kumalizika kwa wakati na kuleta Tija kwa wananchi.

Amesema baadhi ya jamii bado haina uelewa juu ya umuhimu wa kulipa kodi ipasavyo jambo ambalo linasababisha kupotea kwa baadhi ya mapato ya serikali.           

Wakitowa michango kwa Niaba ya Wanafunzi walioshirika mafunzo hayo  Haji Twalib na Mwanahawa Kombo wameipongeza ZRB kwa kuamua kuwafikia katika kisiwa chao juu ya kuwafunza umuhimu wa kulipa Kodi.

Wamesema Taasisi nyingi za Serikali haziwafikii katika kijiji chao jambo ambalo linawakosesha fursa ya kupata elimu ya Ziada itakayosaidia kuimarisha ukuwaji wa Uchumi Nchini.

Aidha wameahidi kuyafanyia kazi mafunzo waliyoyapata kwa kuwafunza wengine ili kuiwezesha serikali kunufaika na vyanzo vya Mapato vya ndani ya Nchini.

Hii ni mara ya Kwanza kwa Bodi ya Mapato Zanzibar ZRB kufanya Safari ya Kutoa Elimu ya Mlipa kodi katika Wilaya ndogo ya Tumbatu ambayo kisiwa chake kipo pembezoni mwa Wilaya za zanzibar.

Na: Fat-hiya Shehe Zanzibar24