Mikakati ya makusudi inahitajika katika kukabiliana na uingizwaji wa mifuko ya plastiki hasa kwa wasafiri wanaonunua bidhaa zisizolipiwa ushuruku ndani ya maduka ya viwanja vya ndege vya kimataifa (duty free shops) na kuingia nayo hapa nchini.

Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee alisisitiza hayo hivi karibuni katika vikao vya Utekelezaji wa Mpango Kazi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais wakati ilipowasilisha taarifa ya Julai 2018 hadi Machi 2019 huko Ikulu ndogo Kibweni.

Katika maelezo yake Dk. Mzee alieleza kuwa ni kawaida kwa wasafiri wakiwemo wageni wanaotoka nje ya nchi kununua bidhaa katika maduka ndani ya viwanja vya ndege hasa vya Kimataifa ambapo kwa kawadia mifuko wanayotumia kutiliwa bidhaa hizo huwa ni ya plastiki.

Aliongeza kuwa wasafisri hao wanapoingia nchini katika viwanja vya ndege huingia na mifuko hiyo na kupita nayo bila ya kuweko kwa uangalifu ama utaratibu maalum uliowekwa kwa ajili ya kuizuia na hatimae kuwaelekeza juu ya athari na marufuku iliyowekwa hapa nchini.

Alisisitiza kuwa ni vyema zikawepo taratibu maalum za kuwafahamisha wasafiri wakiwemo wageni kutoingia na mifuko ya plastiki ili iwe njia moja wapo ya kuendeleza mikakati ya kuzuia uingizwaji na matumizi ya mifuko ya plastiki hapa Zanzibar.

Dk. Mzee alitumia fursa hiyo, kuipongeza Ofisi hiyo kwa juhudi kubwa inayochukua katika kuzuia ungizaji wa mifuko ya plastiki hapa nchini na kusisitiza haja ya taasisi husika kukaza kamba kwani bado wapo baadhi ya wafanyabiashara wakiwemo wadogo wadogo wanaitumia mifuko hiyo masokoni.

“Mimi kwa kawaida nikisafiri nikipita “duty free” huwa na mkoba wangu maalum kwa ajili ya kutilia vitu vyangu ninavyonunua …………..hivyo, mikakati maalum inahitajika katika kuzuia mifuko ya plastiki kuingia nchini”, alisisitiza Dk. Abdulhamid Mzee.

Alieleza kuwa iwapo juhudi za makusudi zitaendelea kuchukuliwa Zanzibar inaweza kufikia malengo yake iliyojiwekea katika kuzuia matumizi ya mifuko ya plastiki kutokana na athari zake kubwa za kimazingira.

Kwa mujibu wa maelezo ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Ofisi hiyo imeendelea kuchukua juhudi za kupambana na uharibifu na uchafuzi wa mazingira kwa kutoa elimu kwa jamii juu ya uhifadhi wa mazingira.

Ofisi hiyo ilieleza kuwa tayari imeshafanya operesheni 90 za kusimamia upigaji marufuku mifuko ya plastiki ambapo kilo 621 za mifuko ya plastiki zilikamatwa na watu 149 wamekamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Zanzibar tayari imeshetangaza rasmi utekelezaji wa sheria namba 49 iliyopitishwa mwaka 2011 ambayo inapiga marufuku uingizwaji na utumiaji wa mifuko ya plastiki hapa nchini.

Ingawa Zanzibar haijafanikiwa kwa asilimia 100 kudhibiti matumizi ya mifuko ya plastiki lakini tayari imepata mafanikio na kupiga hatua kubwa katika kufanikisha suala hilo ambapo hivi sasa mifuko hiyo imeweza kupungua kwa kiasi kikubwa.

Kabla ya kupitishwa kwa sheria hiyo mwaka 2011, mifuko ya plastiki ilikuwa ni tishio kwa mazingira hali ambayo iliondosha haiba ya kisiwa cha Zanzibar ambacho kilikuwa kinasifika kwa rangi ya kijani kutokana na uwepo wa miti na mimea mbali mbali.

Kwa upande wa Tanzania bara mnamo Aprili 10, 2019 Bungeni Jijini Dodoma Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitangaza marufuku ya mifuko ya plaskiti kwa kusema Mei 31, 2019 itakuwa siku ya mwisho kuruhusu utengenezaji, uuzaji, uingizaji na utumiaji mifuko ya plastiki kwa ajili ya kubebea bidhaa za aina yoyote.

Uchafuzi wa mazingira unaotokana na taka za plastiki huathiri na kuharibu mazingira ya miji, ardhi, mito, maziwa, mashambani na hata baharini na hata hivyo, kutokana na kuenea kwa taka hizo, viumbe kadhaa wa baharini huathiriwa na kemikali zitokanazo na taka za plastiki au kwa kula mabaki ya plastiki.

 Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar