Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Hamad Rashid Mohamed amesema Serikali inaandaa sheria zitakazowalazimisha Wafanyakazi wanaopewa fursa za kusomea taaluma ya udaktari nje ya nchi kurudi Zanzibar ili kufanya kazi kizalendo.

Waziri Hamad ameyasema hayo kwa nyakati tofauti alipofanya ziara katika Kitengo cha Matibabu ya Uti wa Mgongo na Kichwa kilichopo Hospitali ya Mnazi mmoja na Hosptal ya Wilaya ya Kivunge Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Amesema kuna tabia iliyojengeka muda mrefu ya Wasomi kupewa nafasi za kusoma nje ya nchi lakini wanapomaliza masomo yao hukataa kurudi nyumbani kufanya kazi.

Amesema hali hiyo huchangia ongezeko la uhaba wa madaktari bingwa katika baadhi ya maradhi na hivyo kupelekea Serikali kupoteza fedha nyingi za kuwahudumia wagonjwa nje ya nchi.

Hivyo Serikali ipo mbioni kuhakikisha kila anayepata fursa za masomo anarudi kwa ajili ya kuwahudumia wananchi wa Zanzibar.

“Haiwezekani mtu anapewa fusrsa ya kusoma nje ya nchi lakini akimaliza tu anatafuta sehemu ya kwenda kufanya kazi nje..Hii sio haki tunaandaa Sheria tuwashitaki Wazazi wake au tukamate mali zake” alisema Waziri Hamad

Aidha Waziri Hamad amekemea lugha chafu zinazotolewa na Madaktari kwa Wagonjwa na kusema kuwa hana muhali kwa Daktari mwenye tabia hiyo

Ameongeza kuwa miongoni mwa mambo yanayomchukiza ni kusikia Wananchi wakilalamika kuhusu Madaktari na Wauguzi wenye tabia ya kutoa lugha chafu kwa wagonjwa huku wakitambua kwamba wagonjwa wanahitaji faraja muda wote.

“Kazi yenu ni nyepesi kukuingizeni Peponi maana munapompa maneno mazuri mgonjwa mnapata thawabu na mnavyomtibu pia mnapata fungu mbele ya mungu na kinyume chake ni dhambi” aliwanasihi Waziri Hamad

Waziri Hamada amewahakikishia Wafanyakazi wa Wizara hiyo mashirikiano ya karibu na kutatua changamoto wanazokabiliana nazo katika utendaji kazi wao.

Miongoni mwa mambo aliyowaahidi ni kupigania Bajeti ya Wafayakazi wanaojihusisha na Utabibu kwa kupaitiwa Sare niform ili waondokane na usumbufu.

“Kama askari wanapatiwa Sare za kuja kazini kwa nini madaktari wao wanunue kwa pesa zao..Hili nakuahidini nitalisimamia na kupatia ufumbuzi” Aliahidi Waziri Hamad.

Awali akizungumza kwa niaba ya wenzake Mratibu wa Kitengo cha Matibabu ya Uti wa Mgongo na Kichwa kilichopo Hospitali ya Mnazi mmoja Dkt. Mohamed Ally amesema toka kuanzishwa kwa kitengo hicho Wagonjwa zaidi ya 800 wamefanyiwa matibabu ya upasuaji yakiwemo ya Mgongo na Vichwa toka kuanzishwa kwake mwaka 2014.

Aidha amefahamisha kuwa kutokana na kufanya matibabu hayo ya upasuaji wamefanikiwa kuokoa zaidi ya Dola za kimarekani Million 20 ikiwa wagonjwa hao wangefanyiwa matibabu nje ya nchi.

Hata hivyo Dkt. Mohamed aliomba Serikali kukiangalia kitengo hicho kwa ukaribu na kukifanya kuwa Taasisi inayojitegema ili kwenda sambamba na mabadiliko ya wagonjwa na utaalam.

Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar 06.03.2018