Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kuikumbusha jamii juu ya hasara na madhara  yanayotokana na Ajira za watoto ili waweze kuishi katika mazingira yenye matumaini kwa ajili ya maisha yao ya baadae.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee,Wanawake na Watoto Maudline Cyrus Castico Ofisini kwake Mwanakwerekwe wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika kuadhimisha siku ya kupinga Ajira za  Watoto ambapo huadhimishwa kila ifikapo tarehe 12. 6 ya kila mwaka.

Alisema Shirika la kazi Duniani (ILO) katika mwaka 2002 lilitoa tamko kwa Jumuiya za kimataifa juu ya kuadhimisha siku ya kupinga Ajira za watoto na udhalilishaji ili waishi katika mazingira bora.

Alifahamisha kuwa suala la ajira za watoto bado linaendelea Zanzibar na jumla ya watoto 25,803 wenye umri kuanzia miaka mitano hadi 17 wamo kwenye Ajira ambapo kati yao wa kiumeni 15,855 na wa kike ni 9,948.

Waziri Castiko ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imechukua hatua mbalimbali katika kukabiliana na tatizo hilo na kuanzisha  Sheria ya ajira Nama11 ya mwaka 2005, sheria ya mtoto ya mwaka 2011, mikakati ya kuwezesha wananchi kiuchumi na miongozo na mipango ya kupambana na ajira kwa watoto.

Hata hivyo alisema pamoja na juhudi zote zilizochukuliwa, takwimu zinaonyesha kuwa suala la Ajira za watoto bado linaendelea kushamiri na jitihada mbali mbali zinahitajika ili kuliondoa au kulipunguza kwa kasi kubwa.

Katika kuadhimisha siku ya kupinga Ajira za Watoto, Waziri Castico ameishauri  jamii kuzingatia matakwa ya kimataifa kuhakikisha wanatokomeza kazi za shuruti, kumaliza utumwa na kuondosha ajira mbaya za Watoto ikiwemo kuwatumia katika vita ifikapo mwaka 2025.

Amewataka  wazazi na walezi kuhakikisha kuwa kila mtoto anapatiwa haki zake za msingi na kuacha tabia ya kuwafanyisha kazi kwa lengo la kuongeza kipato ndani ya familia.

Kaulimbiu  ya siku ya Kimataifa ya kupambana na Ajira za Watoto mwaka huu “Watoto wasifanye kazi kivitendo bali wafanye kazi kwenye ndoto”