SMZ yaendelea kupambana na vitendo vya ukatili Nchini

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imejidhatiti kupambana na vitendo vya ukatili na  udhalilishaji wa wanawake na watoto kwa nguvu zake zote, ambapo takwimu za mwaka 2017/2018 zinaonesha kuwa matukio 1, 091 yalioripotiwa kutoka jeshi la Polisi ukilinganisha na matukio 2, 449 yaliyoripotiwa mwaka 2016/2017.

Hayo ameyazungumza Makamo wa pili wa Rais wa Zanzibar Mhe Balozi Seif Ali Iddi huko katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi chukwani nje kidogo ya mji  wa Zanzibar wakati alipokuwa akiakhirisha mkutano wa kumi na mbili wa Baraza la Tisa la Wawakilishi .

Alisema takwimu hizi hazifurahishi hata kidogo hivyo ijapokuwa jitihada mbali mbali ya  matukio haya yamepunguwa kwa mwaka 2017/2018 kwa  hiyo inaonesha wazi tukijipanga vizuri tunaweza kupunguza vitendo hivi na pia hatimae kumalizika kabisa.

Pia alisema uzoefu unaonyesha kuwa vitendo vya ukatili na udhalilishaji hufanywa na watu wa karibu na familia na jambo la kusikitisha pale watu tunaowaamini kama walimu wa madrasa na Skuli kushiriki kwani matukio haya  zaidi hufanywa kwa watoto kuliko watu wazima , ambapo takwimu kutoka Jeshi la Polisi zinaonyesha asilimia 88.8 ya matukio yaliyopokelewa yalikuwa ya watoto katika mwaka 2017/2018.

Balozi Seif alihimiza viongozi wa Baraza la Wawakilishi  kuwa na tabia ya kupima afya zetu ili tupate kujitambua kwani bado ukimwi upo na unaathiri nguvu kazi ya Taifa na bado hauna dawa hivyo alitoa wito kwa wananchi kuchukua juhudi za makusudi kutumia ipasavyo huduma za upimaji na kutendea haki kauli mbiu ya mwaka huu “Pima virusi vya ukimwi ujue afya yako.

“Juhudi kubwa bado inahitajika kwa jamii katika kupunguza maambukizi tunatakiwa tuwe na tahadhari kubwa kwani maradhi haya hayana dawa.”Alisema Makamo wa Pili.

Na Mwashungi Tahir.  Maelezo