Mjumbe wa baraza la wawakilishi Nadir Abdul-latif Yussuf ameitaka serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuzifungia baa zilizopo Bweni Matrekta kwani baa hizo zimekuwa zikijihusisha na vitendo viovu na wateja wao kufanya uhalifu kwenye maeneo hayo.

Akizungumza katika kikao cha baraza la wawakilishi Nadir amesema baa hizo zimekuwa zikijihusisha na uvunjifu wa sheria za Vileo, na kupiga mziki kinyume na utaratibu uliopangwa.

Amesema hata hivyo Baa hizo zinafanywa madanguro kwani vijana wakike wanauza miili yao pamoja na vijana wa kiume kujihusisha na uuzaji wa madawa ya kulevya kwenye maeneo hayo.

Hivyo Mjumbe huyo  ameiyomba serikali kutokana na kuwepo uovu huo wazifungie  baa hizo ili kuepusha matatizo kwa vijana na wakaazi wa maeneo hayo.

Kwaupande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais Mohammed Aboud ametoa wito kwa Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar kufanya uchunguzi kwenye maeneo hayo ya baa yanayolalamikiwa ili kuwachukulia hatua za kisheria wanaojihusisha na matukio hayo.

Amesema pia Serikali inaunda kamati ya uchunguzi kupeleleza matukio hayo na endapo itajirizisha kuwepo kwa matendo hayo wahusika wa baa hizo watafikishwa kwenye mikono ya sheria.

Nae Katibu wa Mahakama ya Vileo Zanzibar Saleh Ali Abdalla akizungumza na Mwandishi nje ya kikao cha baraza amewataka wakaazi wa Bweni ambao wanaishi karibu na baa hizo kufika mahakamani kuweka pigamizi zao juu ya matatizo ya baa hizo na mahakama itaweza kuchukua hatua stahiki ili kuondosha kero kwenye maeneo hayo.

Amina Omar