Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais  na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  ambaye pia ni mwakilishi wa Jimbo la Chwaka Issa Haji Ussi amesema, makundi ya baraza ndani ya mashehia ni muhimu sana ambayo yapo katika ilani ya Chama Cha Mapinduzi hivyo Serikali inatekeleza ahadi zake katika kuwalinda vijana kama masharti yalivyokubaliwa.

Hayo aliyasema leo huko katika  ukumbi wa Sanaa wa Rahaleo wakati alipokuwa akifungua Mdahalo juu ya ushirikishwaji wa vijana katika siasa na ngazi za maamuzi  kwa vijana wa wilaya ya mjini na kati pamoja na masheha na wawakilishi.

Alisema vijana ndio nguzo ya Taifa hivyo ni vizuri kuwashirikisha katika kutoa maamuzi kwenye siasa  yaliyo mazuri  ambayo yatapelekea kulinda amani ya nchi na kujiepusha na uchochezi.

Aidha aliwataka vijana kuitumia fursa hiyo kwa umakini zaidi na kutoa michango yao pamoja na changamoto zinazowakabili kuzieleza ili ziweze kufanyia ufumbuzi kwa ufanisi na kuweza kupatikana maendeleo.

Alisema kiongozi katika sehemu anayoiongoza hawezi kuongoza peke yake lazima awe na kusikiliza maamuzi ya wenziwe ikiwemo vijana hivyo washirikishwe katia kutoa maamuzi yaliyo sahihi.

“Kiongozi mmoja peke yake hawezi kutoa maamuzi lazima ashirikishe na wenziwe ili apate mawazo na aweze kuyafanyia kazi yakiwemo maamuzi ya vijana yanayofaa”. Alisema Gavu.

Vile vile aliwaomba vijana   kutumia mkutano huo kwa kushirikiana na kuweza kujenga udugu kati ya mabaraza mbali mbali  kwa mawazo watakayoyatoa ili yaweze kutumika kwenye mambo yanayoweza kufaa katika  mambo yaliokuwa mazuri kwenye ngazi zote.

Nae Mwenyekiti  wa Chama cha Wanasheria wanawake ZAFELA  Safia Hijja Abras alisema chama chao kiko mbele katika kuwalinda wanawake na watoto katika masuala ya udhalilishaji na kuhakikisha wanashirikiana na Serikali katika kutolewa maamuzi yanayostahiki kwenye udhalilishaji huo.

Pia alisema lengo kuu la mdahalo huo ni kubadilishana mawazo  katika ushirikishwaji wa vijana katika siasa na ngazi za maamuzi  na kuweza kufanyiwa kazi.

Pia alisema mabaraza yanatoa manufaa makubwa kwa vijana na ndio maana chama cha wanasheria kinashirikiana na Serikali  kwa kuwashirikisha vijana kwenye masuala ya kisiasa kiuchumi na kijamii.

Kwa upande wa masheha wakitoa michango yao sheha wa Shehia ya Sogea Abdullah Mohammed amewataka vijana kuaminiana, kushirikiana na kupendana  ndani ya mabaraza yao pamoja na kushirikiana na masheha ili kuweza kufanya kazi zao kwa ufanisi na kuleta maendeleo yaliyokusudiwa.

Nao washiriki wa mdahalo huo wamesema  Mabaraza ya vijana hawajapewa maamuzi ya kutoa mawazo yao na mapendekezo katika kuendeleleza na kusikilizwa  kwenye kutoa maamuzi pale inapohitajika.

Mdahalo huo wa siku moja  umeandaliwa na Chama cha wanasheria  wanawake ZAFELA  kwa ufadhili wa shirika la Maendeleo la foundation for civil society.

Na Mwashungi Tahir  Maelezo