Mkurugenzi wa halmashauri wilaya ya kusini Unguja Kassim Mtoro Abou amesema tayari kamati ya Halmashauri imeidhinisha jumla ya sh.Milioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa vyoo ambavyo ni muhimu kwa wanafunzi.

Ujenzi huo unatarajiwa kuanza haraka mara baada ya kukamilika kwa taratibu za manunuzi.

Fedha hizo zinatoka katika mfuko wa jimbo la Mbunge wa jimbo la Makunduchi ambazo zilikuwa hazijatumika kwa muda mrefu baada ya mbunge wake kupata ajali huko Morogoro Tanzania Bara.

Aidha Mkurugenzi Mtoro aliupongeza mradi wa kujenga uwajibikaji (PAZA) kwa kutoa nafasi kwa wananchi kuibuwa changamoto mbali mbali zinazowakabili.

”Mradi wa kujenga uwajibikaji (PAZA) ambao unatekelezwa kwa pamoja na (WAHAMAZA) umetusaidia kwa kiasi kikubwa na kutukumbusha majukumu yetu ya kuwatumikiya wananchi”

Diwani wa jimbo la Makunduchi  Zawadi Hamdu alisema hayo ni matokeo ya wananchi wenyewe kupaza sauti zao na kutowa malalamiko mbali mbali katika mambo ambayo ni kikwazo katika kupata maendeleo.

”Ujenzi wa vyoo vya shule ya kusini Makunduchi ni muhimu kwa ajili ya kuweka mazingira mazuri ya wanafunzi na usafi na kujilinda na maradhi mbali mbali’alisema.

Baadhi ya wanafunzi wa shule ya Kusini Makunduchi wamefurahishwa na juhudi zinazochukuliwa na Halmashauri ya Wilaya ya kuvikarabati vyoo hivyo ambavyo vimechakaa sana.

”Tumefurahishwa na taarifa za matengenezo ya vyoo vya shule ambavyo kwa sasa havitumiki tena baada ya kuchakaa huku vyoo viliopo sasa vinavyotumika ni vitatu tu”alisema Samira Ali Khatib.

Naibu katibu mkuu wa chama cha Mapinduzi Abdalla Juma Mabodi katika ziara ya jimbo la Makunduchi aliagiza vyoo hivyo vifanyiwe ukarabati mkubwa na kutengewa jumla ya sh.Milioni 10 ikiwa ni fedha za mfuko wa mbunge ambazo hazijatumika.