Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dodoma, jana ilimpandisha kizimbani aliyekuwa Mkurugenzi wa iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) Paschal Muragili kwa madai ya matumizi mabaya ya madaraka.

Muragili alikuwa Mkurugenzi wa CDA hadi Mei mwaka jana ambapo Rais John Magufuli aliamua kuivunja mamlaka hiyo na shughuli zake kurudishwa Manispaa ambayo kwa  sasa ni Jiji.

Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Dodoma Sosthenes Kibwengu amesema Muragili anatuhumiwa kwa makosa ya matumizi mabaya ya mamlaka, kinyume na kifungu cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na rushwa  cha mwaka 2007.

Mbali na mkurugenzi huyo wa zamani,Takukuru imempeleka pia aliyekuwa fundi sanifu Lemanya Benjamini ambao kwa pamoja walifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Emanuel Fovo   wa mahakama ya Hakimu Mkazi.

Akisoma hati ya mashtaka, Mwendesha mashtaka wa Takukuru  Biswalo Biswalo ameieleza mahakama kuwa washtakiwa walitenda kosa hilo Septemba, 2016.

Hakimu Fovo alitoa dhamana kwa washtakiwa wote baada ya kutimiza masharti ya dhamana ambayo ni pamoja na kila mtu kuweka fedha taslimu Sh 23 milioni au mali isiyohamishika yenye thamani hiyo.</p></div><div><p>Nyingine ni kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika pamoja na kuwasilisha hati zao za kusafiria na kuwa washtakiwa hao hawaruhusiwi kusafiri nje ya nchi bila kibali cha Mahakama.

Kesi itaskilizwa tena Juni 4 mwaka huu.