Naibu mkurugenzi mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali John Mbungo ametoa saa 48 kwa kampuni mbili za ujenzi wa mabwawa ya Manga, Mkata na Kwadugwa wilayani Handeni mkoani Tanga kurejesha Sh736 milioni kutokana na kutozingatia maagizo ya viongozi kuhusu ujenzi huo.

Mkandarasi mshauri Don Consult Ltd na mkandarasi mjenzi Tansino walipewa wiki mbili na Rais John Magufuli tangu Agosti 2017 kuhakikisha wanamaliza ujenzi huo kutokana na kujenga chini ya kiwango lakini hadi leo Jumanne Oktoba 8, 2019 wameshindwa kutekeleza agizo hilo.

Katika ziara yake wilayani Handeni, Magufuli aliagiza uongozi wa mkoa kusimamia ujenzi wa mabwawa hayo kwa mkandarasi kutumia fedha zake mwenyewe na kuagiza Sh1.2 bilioni zilizobaki zisitolewe mpaka Serikali itakaporidhishwa na ujenzi huo utakapokamilika.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Mbungo amesema tangu wakati huo hadi sasa mradi haujakamilika kama inavyotakiwa, taasisi yake ilipewa kazi ya kufuatilia na kubaini upungufu katika ujenzi, “wahusika wamekiri makosa yao baada ya kukamatwa na Takukuru.”

Amesema hadi sasa Sh2.8 bilioni zimelipwa kwa wakandarasi hao kwa nyakati tofauti na kwamba Sh1.2 bilioni hazijalipwa kutokana na Serikali kuzizuia baada ya kupata mashaka ya ubora wa miradi hiyo.

katika fedha hizo Wakandarasi hao wanatakiwa kurudisha Sh736 milioni ambazo zimebainika kutumika vibaya katika ujenzi wa mabwawa hayo.

“Kuanzia Oktoba 8 na 9, 2019 tunawataka makandarasi hao kurejesha fedha hiyo,” amesema Mbungo.

Mkuu wa wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe amesema kuna upungufu katika ujenzi wa miradi hiyo, akibainisha kuwa walitakiwa kujenga vituo 48 vya kuchota maji lakini vimejengwa 15 huku 33 vikiwa bado na malipo tayari yameshafanyika.

Kuhusu upungufu katika mabwawa hayo mkurugenzi halmashauri ya wilaya Handeni, Wiliam Makufwe amesema, “bwawa la Manga lipo chini ya kiwango na lilivunjika, la Mkata haliingizi maji vizuri na lipo chini ya kiwango na Kwandugwa linavuja kutokana na kuwepo nyufa kwenye kuta zake.”

Mbunge wa Handeni Vijijini (CCM), Mboni Mhita amesema upo mradi mwingine wa HTM umefanyiwa upembuzi yakinifu na kuwataka wananchi kutokuwa na wasiwasi.

Chanzo: mwananchi