Wananchi wametakiwa kujitokeza kwa wingi katika zoezi la kusajili laini  kwa alama za vidole vidole ili kuepusha udanganyifu katika mitandao

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya uhamasishaji kwa watumiaji wa simu za mikononi kusajili kwa alama za vidole katika mnara wa Mapinduzi Square,   Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharib Hassan Khatib Hassan amesema” Zoezi la usajili wa laini kwa alama za vidole linaratibiwa na serikali na tutumie technologia hii kwa manufaa ya serikali zote mbili na kuzingatia muda uliowekwa na mamlaka husika”

Aidha amesema kufanya hivyo ni kuweka nchi katika hali ya amani na usalama zaidi na kuwataka wasimamizi wa zoezi hilo kuengeza muda wa usajili katika maeneo yote ya Mkoa wa Mjini Magharibi ili wananchi wote waweze kusajili laini zao bila ya usumbufu wowote.

Kwa upande wake muwakilishi wa makampuni ya simu kwa Zanzibar Nd. Mohammed Baucha amewataka wananchi ambao bado hawajasajili laini zao kufika katika maduka yao kwa ajili ya kusajili laini zao kwa alama za vidole wasingoje muda wa mwisho wa zoezi hilo.

Amesema kuwa baadhi ya wahudumu wanaosajili wamekuwa wakisajili kwa kuwatoza pesa wananchi ilihali zoezi hilo ni bure kabisa kusajili.

“Lengo la kuweka uzinduzi huu ni kutaka kufikia asilimia kubwa ya watu wote kusajili laini zao kabla ya tarehe 30 disemba” amesema Baucha.

Naye Kaimu Mkurungenzi kutoka Nida Nd. Hassan Haji Hassan amesema changamoto kubwa wanayokumbana nayo ni pamoja na wananchi kuhama maeneo bila ya barua ya sheha ambapo katika usajili lazima kuwepo na muhuri wa sheha  pamoja na kubadilisha namba za simu na kuwaomba makampuni ya simu kuwasaidia katika hilo.

Sambamba na hayo amewataka wananchi waliokuwa bado hawajaenda kuchukuwa vitambulisho vyao kwenda katika ofisi za Nida  na za wilaya kwenda kuchukuwa vitambulisho vyao ili waweze kuondokana na usumbufu wa kusajili laini zao kwa alama za vidole.

Kauli mbiu katika uzinduzi huo wa usajili wa laini kwa alama za vidole ni “HAACHWI MTU NYUMA KAMILISHA USAJILI”