Mwanariadha bingwa wa walemavu wa Ubelgiji Marieke Vervoort Jumanne alikatiza uhai wake kwa njia ya kuuliwa ili kuondolewa maumivu akiwa na umri wa miaka 40.

Kuuliwa ili kuondolewa maumivu ni njia ya kisheria nchini Ubelgiji na mwanariadha huyo alitangaza nia yake baada ya michezo ya Olimpiki ya Rio mwaka 2016 kwamba atatumia njia hiyo kama hali yake itakuwa mbaya na kumpa mateso.

Image result for marieke vervoort disease

Lakini alisema kwa wakati huo michezo ilimpa sababu ya kuendelea kuishi. Vervoort alisumbuliwa na ugonjwa wa kuzorota kwa misuli ambao unamsababishia maumivu makali, na kupooza miguu na kumfanya ashindwe hata kulala vizuri, na kidogo kidogo maisha yake yakawa ya mateso.

Aligunduliwa ugonjwa huo akiwa na miaka 14 lakini Vervoort alikuwa akipenda michezo, na kucheza mpira wa kikapu wa viti vya magurudumu, kuogelea na mbio za triathlon. Alishinda dhahabu mita 100 na fedha mita 200 kwenye mbio za viti vya magurudumu kwenye michezo ya olimpiki ya London 2012, pamoja na fedha mita 400 na shaba mita 100 nchini Brazil miaka minne baadaye.