TFF yaendelea kupokea zawadi Ubingwa wa ligi kuu ya Soka Zanzibar

Kamati teule ya TFF ya chama cha mpira wa miguu Zanzibar (ZFA) imendelea kupokea zawadi za Ubingwa wa Ligi kuu Soka ya Zanzibar kwa msimu wa mwaka 2017-2018 ambazo zitatolewa rasmi Oktoba 18, 2018 kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii utakaochezwa kati ya Bingwa wa ligi kuu ya Zanzibar ambao ni JKU dhidi ya Bingwa wa Kombe la FA ambayo mashindano yake yanasubiri fainali kati ya KMKM dhidi Jamuhuri kutoka kisiwani Pemba.

Akikabidhi zawadi hizo Afisa Uhusiano wa Kampuni ya ZAT Ali Juma (Ali Raza) amesema kutokana na kuguswa na Michezo wameona ipo haja kusaidia zawadi hizo kwa Bingwa na Makamu Bingwa wa ligi kuu ya Zanzibar.

Aidha amewaomba Wadau wengine wasaidie Michezo ili kuendana na kasi ya Maendeleo ya Michezo  inayofanywa na  Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein.

Kwa upande wake Katibu wa Kamati ya Mashindano kutoka ZFA Alawi Haidar Foum amesema zawadi hizo zitatumiwa kama zilivyokusudiwa huku akiwaomba wadau wa Soka kufuata vyema kalenda ya ZFA ili kuendana na wakati.

‘’kamati imeona kuna haja ya kuwatunuku zawadi kwa mabingwa wetu hivyo tutawakabidhi hizo zawadi kama zilivyokuja ila bado hatujaridhika sana sisi kamati bado tunaendelea kuwatafuta wadhamini  kuwapatia washindi wetu wa ligi kuu ya Zanzibar ‘’ Alisema Alawi Haidar.

Kampuni ya ZAT imekabidhi zawadi Kombe kubwa, Medali 30 za Dhahabu kwa Bingwa wa Ligi kuu ya Zanzibar Medali 30 za Fedha kwa Makamo Bingwa wa Ligi kuu ya zanzibar huku wakiahidi kutoa Jezi, Mipira, Vifaa vyengine vya Michezo pamoja na Fedha Taslim kwaajili ya Zawadi za Bingwa na Makamu Bingwa wa ligi kuu ya zanzibar msimu uliopita wa mwaka 2017/2018.