Timu ya taifa Kenya yafuzu AFCON

Timu ya taifa ya mpira wa miguu Kenya, Harambee Stars imefuzu kushiriki michuano ya Mataifa Bingwa Barani Afrika (AFCON) mwaka 2019.

Thibitisho kwamba Timu ya Taifa Harambee Stars imefuzu kwa michuano hiyo ya 2019 lilitangazwa siku ya Ijumaa baada ya kikao kisicho cha kawaida cha siku nzima cha Kamati Kuu ya Shirikisho la Kandanda Barani Afrika (CAF) jijini Accra, Ghana.

Kikao hicho cha Ijumaa kilithibitisha uamuzi wa kuitupa nje timu ya taifa ya Sierra Leone kutoka kwa michuano inayoendelea kwa sasa kutokana na shirikisho lao kupigwa marufuku na chama chake cha Soka kupigwa marufuku na Shirikisho la soka duniani FIFA.

Sierra Leone, ambayo ilikuwa katika kundi la F la kufuzu pamoja na Kenya, Ghana na Ethiopia, sasa haitashiriki michezo yake mitatu ya mwisho.

Huku ikiwa imesalia mechi moja ya makundi kukamilika, Shirikisho la CAF liliafikia uamuzi wa kufutilia mbali matokeo yote yaliyohusisha taifa hilo la Afrika Magharibi na hivyo kuliacha kundi hilo na timu tatu pekee.

Sierra Leone ilikuwa imecheza tu mechi mbili katika kampeini yao na kwa sababu haikuwa imekamilisha nusu ya mechi zote za kufuzu, Shirikisho la CAF liliamua kufutilia mbali matokeo yote ya awali yaliyohusisha taifa hilo kulingana na kanuni za kufuzu.

Michuano hiyo ilipangiwa kufanyika Cameroon mwaka ujao lakini taifa hilo lilipokonywa nafasi hiyo Ijumaa kutokana na kucheleweshwa kwa ujenzi wa viwanja na miundo mbinu mingine muhimu.

CAF wanatarajia kuteua mwenyeji mpya kufikia mwisho wa mwezi huu.

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ameipongeza timu hiyo ya taifa na kusema kufuzu kwa timu ya Taifa kwa kinyanganyiro hicho barani kwa mara ya kwanza katika muda wa miaka 15 ni ufanisi wa kusisimua kwa wapenda soka nchini humo.

Ameahidi kuiunga mkono kikamilifu timu hiyo.

Sehemu ya ujumbe wa CAF ikionyesha msimamo kwenye Kundi F kwa sasaSehemu ya ujumbe wa CAF ikionyesha msimamo kwenye Kundi F kwa sasa

“Ufanisi wa timu yetu ya Taifa ni ishara ya mabadiliko katika michezo yetu. Tunajivunia kile vijana wetu wanafanya kuimarisha viwango vya mchezo huo nchini,” amesema Rais Kenyatta.

Rais Kenyatta amesema Serikali kupitia Wizara ya Michezo itaendelea kuiunga mkono timu ya Taifa ya Soka inapojiandaa kwa kindumbwe-ndumbwe hicho barani.

“Tunajua mnaweza kushinda taji hili. Nawahakikishia usaidizi wangu na Serikali itafanikisha na kuwapa rasilimali zinazohitajika kuhakikisha mmejiandaa vilivyo kwa kazi iliyo mbele yenu,” Rais Kenyatta amesema.

Awali, Waziri wa Michezo Rashid Echesa, kupitia akaunti yake ya Twitter Twita aliipongeza timu ya taifa kwa kufuzu.

“Kinyang’anyiro hiki kimetuhepa kwa muda wa miaka 15. Nawashukuru vijana wetu kwa kupambana vilivyo dhidi ya timu zote katika kundi lao na kufuzu kuiwakilisha Kenya,” Waziri alisema.

Katibu katika Wizara ya Michezo, Balozi Kirimi Kaberia alisema wanamichezo wa Kenya waume kwa wanawake ni raslimali muhimu ya taifa na akaiihimiza timu ya hiyo ya Soka Harambee Stars kulenga ufanisi katika kinyanganyiro hicho.

Chanzo BBC.