Serikali imeipiga marufuku Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kufunga maduka na biashara za watu kwa kisingizio cha kutolipa kodi.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango jana Desemba 30, 2018 wakati akitoa taarifa ya hali ya uchumi wa Taifa na utekelezaji wa bajeti ya Serikali katika nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha wa 2018/19.

“Utaratibu wa kumfungia biashara mfanyabiashara anayedaiwa kodi ili kumshinikiza alipe sasa usitishwe mara moja, isipokuwa kwa wakwepa kodi sugu na hapo lazima kuwe na kibali cha kamishna wa mkuu wa TRA, nataka mjikite katika kutoa elimu siyo vitisho,”amesema Dkt. Mpango.

Kwa upande mwingine, Waziri Mpango amekemea matumizi mabaya ya lugha, vitisho na ubabe dhidi ya walipakodi wenye historia nzuri akitaka yasipewe nafasi na itakapothibitika mtumishi wa TRA amekwenda kinyume awajibishwe kwa kuzingatia tararibu za kiutumishi.