Rais wa Marekani Donald Trump ameashiria kufanya mkutano binafsi na rais wa China Xi Jinping kujadili mzozo wa kisiasa unaoligubika eneo la Hong Kong.

Katika ujumbe kwenye twitter, Trump amesema hana shaka hata kidogo kwamba Bwana Xi anaweza kutatua kwa huruma mzozo wa Hong Kong.

Amehusisha pia maandamano hayo na mpango wa biashara wa Marekani na Beijing, wakati hali ya wasiwasi wa kibiashara ikiendelea.

Matamshi ya Trump yanajiri baada ya maandamano ya wiki kadhaa ya kutetea demokrasia yaliozushwa na upinzani kupinga mswada wa kuhamishwa kwa wahalifu kushtakiwa nje ya Hong Kong.

Wakosoaji wanahofia mswada huo huenda ukaifanya Hongkong kuzidi kuwa chini ya udhibiti wa China.

Mswada huo umesitishwa kwa sasa, lakini maandamano yamegeuka na kuwa vuguvugu la kuunga kwa ukubwa demokrasia.

Hong Kong ni sehemu ya China chini ya mfumo wa “Taifa moja, mifumo miwili” inayoipatia mamlaka ya juu ya kujitawala.

Ina mfumo wake wa sheria na mahakama na ina uhuru kadhaa usiokuwepo katika eneo kuu – Mfano Hong Kong na Macau fondio maeneo ya pekee katika ardhi ya China ambapo watu wanaruhusiwa kukusanyika kukumbuka maandamano ya bustani ya Tiananmen.