Mbunge wa zamani wa Singida Mashariki, aliyevuliwa wadhifa huo hivi karibuni, Tundu Lissu ameanza rasmi harakati za kupigania ubunge wake mahakamani baada ya kufungua shauri la maombi ya kibali cha kupinga uamuzi huo wa kumvua ubunge.

Mwanasheria huyo mkuu wa Chadema ambaye yuko nchini Ubelgiji alikokuwa akipatiwa matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu ambao hadi sasa hawajajulikana, alifungua rasmi shauri hilo jana.

Lissu ambaye pia alikuwa Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, amekuwa nje ya nchi kwa matibabu baada ya kunusurika katika jaribio hilo la mauaji lililotokea Septemba 7, 2017 akiwa nje ya makazi yake huko Dodoma.

Amefungua shauri hilo chini ya hati ya dharura, kupitia kwa kaka yake Alute Mughwai ambaye amempa mamlaka ya kisheria kufanya hivyo.

Uamuzi wa kumvua Lissu ubunge ulitangazwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai Juni 28, wakati akiahirisha mkutano wa 15 wa Bunge, huku akitaja sababu mbili.

Alizitaja sababu hizo kuwa ni kushindwa kuhudhuria vikao vya Bunge kwa muda mrefu bila kumjulisha Spika kwa maandishi mahali aliko na sababu ya pili ni kutokujaza taarifa za mali na madeni kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.