Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeahirisha kesi inayowakabili
Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko hadi Januari 3, 2019 hali itakayopelekea watuhumiwa hao kusalia Gerezani kwa kipindi chote cha Sikukuu ya Krismas na mwaka mpya.

Mahakama imetoa uamuzi huo leo Desemba 21 katika kesi inayowakabili viongozi wakuu wa Chama hicho, wakiongozwa na Mweneyekiti wao Freeman Mbowe na baadhi ya viongozi wenzake wa juu pamoja na wabunge.

Kwa mujibu wa wakili wa serikali, Simon amedai kuwa hawana taarifa ya kinachoendelea mahakama ya Rufaa hivyo waliomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Kwa upande wake, wakili wa upande wa washtakiwa Faraja Mangula walieleza baadhi ya Mawakili akiwemo Peter Kibatala na Sheck Mfinanga wamepata dharura hivyo wanaomba mahakama ipange Januari 4, 2019.

Kufuatia uamuzi huo wa mahakama, Mbowe na Matiko wamerudishwa gerezani baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwafutia dhamana Novemba 23, 2018 kwa kukiuka masharti ya dhamana ikiwemo kutoka nje ya nchi bila kibali.