Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo imeanza kutekeleza maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. John Pombe Magufuli kubadili jina la uwanja wa Taifa kumuenzi Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Hayati Benjamini Wiliam Mkapa.

Taarifa hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Michezo wa Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Yusufu Singo, na kueleza kuwa mchakato umeshaanza na wameshaliondoa jina la zamani ili kuweka jina la Benjamini Mkapa, kwa maelekezo ya Waziri wa Michezo na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo.

” Baada ya maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh Dkt John Pombe Magufuli kutaka uwanja huu ubadilike ili tuweze kumuenzi Rais wa awamu ya Tatu, Hayati Benjamini Mkapa, tayari Waziri mwenye dhamana ya michezo na katibu Mkuu wa Wizara ya michezo, wameelekeza tuanze shughuli hiyo mara moja na tumeanza kuliondoa jina la zamani la ‘National Stadium.” Alisema Singo.

Singo ameongeza kuwa baada ya kuliondoa jina la zamani la uwanja huo, lakini kuna changamoto kidogo ya kuliweka jina jipya hivyo wanasubiri kukutana na wataalam wa Wizara, huku mafundi wakiwa tayari wanaendelea na ujenzi kwenye eneo husika.