Uchambuzi athari za Muhali.

 

MUHALI si jambo zuri na jema kwenye suala zima la uajibikaji , hasa katika taasisi za Serikalina hata sekta binafsi, hususan kwa wale waliopewa dhamana ya kuongoza pamoja na kutoa maamuzi ndani ya tasisi zao.

suala hilo pia husababisha na kuchangia kwa kiasi kikubwa uyumbishwaji na ukiukwaji wa misingi ya sheria, sambamba na kukwaza utekelezaji wa majukumu katika sekta mbali mbali zinazotoa huduma kwa jamii.

Muhali ikiwa inafanya kazi sambamba na rushwa ,kutowajibika ipasavyo kwa watumishi wa umma katika sekta mbali mbali ambazo zimepewa dhamana  katika ngazi ya maamuzi na utoaji wa huduma za jamii.

Mara nyingi watu wa aina hii hawaangalii sheria wala taratibu zilizopo ,isipokuwa kuweka mbele muhali, ubinafsi, udini na ukabila na kuweza kuhujumu haki za wengine.

Tufahamu kuwa muhali ni adui mkubwa wa haki na husababisha chuki, fitina,majungu,migogoro na hata kuifanya nchi kutofikia katika malengo yake iliyojiwekea, kwa maendeleo ya wananchi wake na taifa kwa ujumla.

Hebu tutafakari kwa kina na turudi katika misingi ya sheria na utawala bora na hata misingi ya kidini ,hivi kweli kuweka mbele muhali ,rushwa na kutowajibika vinaweza kuleta tija na mtazamo mwema kwa jamii?

Kwa jibu la haraka haviwezi kuleta faida kwa Taifa bali huchangia kwa kiasi kikubwa ukandamizaji ukiukwaji wa haki na kuifanya nchi kudidimia katika dimbwi la umasikini .

Pia tufahamu kuwa, kutokufuata misingi ya sheria na utawala bora katika utoaji wa huduma ,maamuzi na upatikanaji wa haki za watu ,ndio husababisha baadhi ya watu kuchukua hatua mikononi mwao huku wakidai kwamba Serikalini hakuna sheria na hata kama zipo basi hazifwati.

Pamoja na hatua zinazochukuliwa na wananchi hao,kwa kuwaadhibu wanaofanya vitendo viovu kamavile wizi, ubakaji ,ulawiti wa watoto wadogo,pamoja utumiaji wa madawa ya kulevya, kwa kuwaadhibu vikali kwa vipigo na wakati mwengine kuwaua kabisa bila hata kuwafikisha katika mkono wa sheria.

Kwani hudai kuwa hata wanapo wapeleka katika sheria, hakuna lolote linalofanywa na hiyo sheria, matokeo yake wahalifu hao huendelea kufanya vitendo hivyo viovu katika jamii inayowazunguuka ,wakiamini kuwa hawawezi kuhukumiwa kutokana na kutegemea nguvu fulani inayowalinda na hapo huendelea na uovu huo bila ya wasiwasi na uoga katika nyoyo zao.

Tufahamu kuwa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla ni kama nchi nyengine za dunia zinazoongoza raia wake kwa kufuata misingi ya sheria, kanuni na utawala bora  katika kuleta maendeleo ya Taifa .

Lakini hebu tujiulize ! Hivi kama sheria na kanuni tunazozitunga wenyewe kupitia  vyombo vyetu vya kutunga sheria na tukaviamini juu ya kutuekea miongozo ya kutuongoza, tunazipa mgongo na kuweka mbele muhali, rushwa kuwa ndio dira ya kutuongoza, kweli huo ndio utakuwa utawala bora na demokrasia?

Kwa muono wa haraka tunaweza kusema hapana , kwani utawala bora na kidemokrasia, ni utawala unaoendeshwa kwa kufuata misingi ya sheria na kanuni bila ya kukiukwa na mtu yoyote ,awe wa ngazi yoyote katika uongozi,ndio tutasema kuwa huo ndio utawala bora na demokrasia.

Ikumbukwe kuwa muhali ndio huficha na kuzuia haki za watu na kuharibu mustakbali mzima wa maendeo ya taifa na hata kuwajenga wananchi kotowaamini viongozi wao, jambo ambalo linakwamisha kasi ya maendeleo ya taifa.

Ni wajibu wa kila mmoja wetu kusisimamia imara na kumpiga adui huyu mkubwa wa haki za watu, ili tuweze kujenga mustakbali mzuri wa maisha yetu kwa ujumla.

Sina lengo la kualumu, isipokuwa nina nia njema kabisa ya kuwakumbusha waungwana wenzangu kuwa, wakati umefika sasa kwa wale waliopewa dhamana ya kuongoza na  kusimamia haki kwa kufuata misingi ya sheria isitoweke.

Ni dhahiri kuwa, iwapo tutafuata taratibu tulizojiwekea tutaweza kumshinda adui muhali na kufanya haki na uadilifu kutawala,mwenye kudhulumiwa atapata haki yake na mwenye kudhulumu atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria .

Kufanya hivyo kutasaidia kuwajenga na kuwajaza imani wananchi njuu ya viongozi wao ,katika taasisi zilizopewa dhamana ya kuongoza na utoaji wa hukumu juu mambo mbalimbali yanafanywa katika jamii.

Bila shaka likisimamiwa hili kwa dhati na uadilifu kila mmoja akajua wajibu wake basi chuki,fitina majungu miongoni mwa jamii zetu yatapungua na hata kutoweka kabasa .

Kwa wale waliopewa dhamana ya kuongoza ,wakati umefika sasa wavue majoho waliojivisha katika ukiukwaji wa sheria na taratibu za nchi hatimae wajipange upya katika kuwa viongozi na sio bora viongozi.

Utekelezaji wa hayo utaimarisha silka, hulka na utamadini wa taifa letu na yataweza kuleta muangaza nchini mwetu, mithili ya taa ya karabai inavoangaza gizani,na wageni kuamini Zanzibar na Tanzania kwa ujumla ni darasa lao la kujifunza yalio mazuri kutoka kwetu.

Zanzibar bila muhali, rushwa na kutokuwajibika inawezekana, kila mtu atimize wajibu wake ili tufikie malengo tulio jiwekea.

 

Na Ibrahim Makame.