Wahenga walisema mcheza kwao hutunzwa, ndivyo tunavyoweza kusema kwamba SMZ imecheza kwao na inafaa itunzwe hasa kwa hili la ujenzi wa mitaro kwani imecheza kama Pele.

Vizazi vya millennia (Millenials) na vizazi Z (Generation Z ) havikuwahi kumuona gwiji na guru la kusakata kandanda kwa mchezo wa kibrazili (Samba) Edson Arantes do Nascimento maarufu Pele akicheza soka la ushindani, lakini vizazi hivi vya akina Messi, Ronaldo na Mbappe wanamfahamu Pele ambaye hadi sasa yuko hai. Kwa kifupi hakuna mpenda soka asiyeyajua mafanikio ya Pele mwenye tepe tatu za Dunia kwa maana ya kuchukua kombe la Dunia mara tatu 1958, 1962 na 1970.

Mafanikio ya Pele ndio mafanikio ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika ujenzi wa Mitaro katika mji wa Zanzibar.

Mimi binafsi nayaita mafanikio ingawaje ujenzi unaendelea na bado haujakamilika lakini palipofikiwa panatosha kupatathmini. Pita pale kwa Binti Hamran Mpendae, viunga vile vilikua uwanja wa maji katika kila msimu wa masika na kuwafanya wananchi wa eneo lile kuwa na kumbukumbu mbaya ya kuingiliwa na maji ndani kila msimu wa mvua unapofika. Msimu uliopita hadithi iligeuka, pakavuuu kama sio masika, mwenye macho haambiwi tizama.

Ukweli wa mambo ni kwamba hakuna asiyejua adha ya mafuriko, si pale Mwanakwerekwe, si kule Sebleni, kwengineko Nyerere, kule kiziwa maboga na mwisho wa matatizo kule njia panda ulaya kunakokaribishwa watalii, ilikua haihadithiki, haisimuliki, mtalii kabla hajafika kwenye fukwe mwanana na hajaona kijani kibichi na mashamba ya viungo kule kizimbani, anakaribishwa na ufukwe mpya pale barabarani Kiembe Samaki.

Makubwa yamefanywa, la mitaro Serikali imejijengea uaminifu na heshima (Trust and Respect) kwa wazanzibar. Dkt. ALI MOHAMMED SHEIN, Rais wa Zanzibar kwa hili naye amejijengea Uaminifu na Heshima.

Bahati mbaya sana, nasema Bahati mbaya sana, Utamaduni wa kusifu jambo jema umeondoka kwa vizazi vyetu lakini la mitaro ni moja ya jambo jema na ni uongozi unaoacha alama. Professor Marshall Sashkin katika kitabu chake ‘Leadership that Matters’ ameeleza vipi unamjua kiongozi mleta mageuzi na mwenye kuacha alama. Ukisoma kitabu hicho na ukilitizama la mitaro utaelewa.

Ngoja niweke nukta kwa kukumbusha suala la kuzingatia na lisiloepukika. Lazima Manispaa za Mkoa wa Mjini Magharibi zijiandae kiuwezo kuhudumia mitaro hiyo. Muda ndo huu kuzijenga na kuzipanga upya kwa kuzingatia uweledi Idara zinazoshughulikia huduma za mitaro kwenye manispaa zetu. Kuambizana kumo.