Ushahidi kesi ya Wema Sepetu kuanza kutolewa Machi 18

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepanga Machi 18, 2019 kuanza kusikiliza ushahidi katika kesi ya kuchapisha video ya ngono inayomkabili mlimbwende wa Tanzania mwaka 2006, Wema Sepetu.

Uamuzi huo umetolewa leo Februari 21, 2019 na Hakimu Mkazi, Maira Kasonda baada ya upande wa mashtaka kumsomea maelezo ya awali mshtakiwa huyo.

Wema  anakabiliwa na shtaka moja la kuchapisha video ya ngono na kusambaza katika mtandao wa kijamii wa Instagram kinyume cha sheria.

Wakili wa Serikali, Glori Mwenda ameieleza mahakama hiyo kuwa kesi ilikuja kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa maelezo ya awali na upande wa mashtaka wapo  tayari kumsomea.

Baada ya upande wa mashtaka kueleza hayo, wakili wa Wema, Ruben Simwanza amedai hana pingamizi juu ya mteja wake kusomewa maelezo hayo.

Baada ya upande mashtaka kumsomea maelezo hayo, hakimu aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 18, 2019.

Wema  alifikishwa  kwa mara ya kwanza Kisutu  Novemba Mosi, 2018 kujibu shtaka hilo.

Hata hivyo, mshtakiwa huyo yupo nje kwa dhamana.

Katika kesi ya msingi, Wema anadaiwa Oktoba 15, 2018 katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam alichapisha video ya ngono na kuisambaza katika mtandaoni wake wa kijamii wa Instagram.