Mkutano wa ngazi ya juu kuhusu ukimwi jana ( alhamis) uliingia katika siku yake ya pili ambapo viongozi mbalimbali wakiwamo Mawaziri na Naibu waziri wanaohusika na masuala ya afya wameendelea kuelezea nini ambacho nchi zao zinatekeleza katika kukabili na kudhibiti maambukizi mapya ya virusi vinavyo sababisha ukimwi pamoja na huduma wanazopatiwa watu ambao wamekwisha kuathirika na kuugua.

Mmoja ya nchi ambayo iliwasilisha mafanikio, changamoto na mwelekeo wa baadaye katika kukabiliana na janga la ugonjwa wa ukimwi, ugonjwa ambao jumuiya ya kimataifa umejiweka lengo la kuutokomeza ifikapo mwaka 2030 ili kuwa ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Juhudi za Tanzania dhidi ya Ukimwi, zilielezwa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dr. Hamis A Kigwangalla (Mb). Ambaye katika maelelezo yake, amesema, Tanzania inaamini kuwa inawezekana kufikia hali ya kutokuwa na maambukizi mapya, kumaliza ubaguzi na unyanyapaa, na kuwa na kiwago sifuri cha vifo vinavyohusiana na ukimwi fikapo mwaka 2030.

Hata hivyo anasema, ili kufikia hatua hiyo au mafanikio hayo, mambo kadhaa yanapashwa kufanyika, yakiwamo ya uimarishwaji wa elimu ya kinga, vijana na jumuiya kwa ujumla kufundishwa mbinu za kuepukana na tabia hatarishi ambazo zinachangia ongozeko la waathirika na kuhakikisha upatikanaji kirahisi wa za dawa na ambazo zitakuwa za gharama nafuu.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri ambaye anaongoza ujumbe wa Tanzania katika mkutano huu, amekwenda mbali zaidi kwa kusema pia patahitajika kupunguza vifo vitokanavyo na ugonjwa wa Kifua Kikuu kwa watu wanaoishi na virusi vya ukimwi, kujadili masuala ya jinsia pamoja na mila na tamaduni, kutenga raslimali za kutosha kwaajili ya watu wenye mahitaji wakiwamo vijana, kuwa na viwanda vitakavyoweza kuzalisha dawa.

Akizungumza baadhi ya mafanikio ambayo Tanzania imekwisha kuyafikia katika kukabili tatizo la ukimwi, Naibu Waziri ameyataja baadhi ya mafanikio hayo kuwa ni pamoja na kupunguza maambukizi mapya kutoka 140,000 mwaka 1990 hadi kufikia 63,000 mwaka 2014. Vile vile vifo vitokanavyo au vinavyosaabishwa na ukimwi pia vimepungua kwa asilimi 40 katika kipindi hicho.

Akaeleza pia kwamba hata watu wanaopatiwa huduma ya matibabu nayo imeongezeka kufikia asilimia 60 huku ongezeko likiwa kwa watoto na hasa baada ya kupitisha mpango unaotambulika kama Option B+ miaka sita iliyopita.

Kuhusu kupungua kwa raslimali fedha hususani kutoka kwa wafadhili, Dr. Kingwangalla, amesema katika kukabiliana na changamoto hiyo, na kwa kuzingatia wito wa jumuiya ya kimataifa kupanua wigo wa mapato ya ndani, serikali ya Tanzania ilianzisha Mfuko wa ukimwi, (AIDS Trust Fund) mfuko anaosema hadi sasa serikali ndiyo imekuwa mchangiaji mkuu, ingawa pia kwamba sekta binafsi nayo inatazamiwa kuchangia.

Akasema sehemu au nusu ya fedha hizo (55%) itakwenda kusaidia upatikanaji wa huduma na kuongeza kuwa juhudi hizo za serikali pia zimesaidiwa na ushirikiano baina ya Tanzania na nchi nyingine rafiki pamoja na mashirika ya kimataifa na akatumia fursa hiyo kuwashukuru wale wote ambao wanachangia juhudi za serikali.

Kuhusu mipango mingine ambayo serikali inaendelea nayo , Naibu waziri alikuwa na haya ya kueleza “ baada ya kuwa tumeanza utaratibu wa kupima na kutibu kwa baadhi ya wilaya chache nchini, tunakusudia kuisambaza huduma hiyo lakini itakuwa ni kwa hatua ili kutoa nafasi ya kuwajengea uwezo watoaji wa huduma ya afya, kuhuisha mifumo ya usambazaji wa vifaa ikiwa ni pamoja ushiriki wa jamii ili iweze kupokea na kuukubali mfumo huu mpya wa utoaji wa huduma” ameeleza Naibu Waziri.

Akasisitiza zaidi kwa kusema ingawa ugonjwa wa ukimwi umeendelea kuwa changamoto kubwa kwa maendeleo ya nchi ambapo inakadiriwa watu 1.5 milioni wameathirika, huku mzingo mkubwa ukiwaelemea wanawake na vijana hasa watoto wa kike, serikali ya tanzania itaendelea na jitihada zake za kuhakikisha inafikia lengo la kutokuwa na maambukizi mapya, kutokomeza unyanyapaa na ubaguzi, na vifo vinatokanavyo na ukimwi.

Katika hatua nyingine amesema ili kutorudisha nyuma mafanikio ambayo Tanzania imeyafikia hadi sasa pamoja na nchi nyingine kusini mwa Jangwa la Sahara Jumuiya ya Kimataifa inaombwa kusaidia jitihada zinazofanywa na serikali za nchi hizo za kuwa na mapato yake yenyewe ya kugharamia huduma za afya kwa wagonjwa wa ukimwi na pamoja na huduma nyinginezo badala ya kuziachia kabisa jukumu hilo.