Kwa mujibu wa jarida maarufu la masuala ya fedha la Forbes, Mohamed Dewji ana utajiri wa dola bilioni 1.5.

Mo mwenye umri wa miaka 43 ndiyo tajiri namba moja Afrika Mashariki, na pia ni miongoni mwa matajiri wa umri mdogo zaidi Afrika.

“Alinunua viwanda vya nguo na mafuta vilivyokuwa vinamilikiwa na Serikali kwa bei ndogo na kuvifanya viwe na faida zaidi kwa kutumia mtindo wa kisasa wa menejimenti,” inaongeza ripoti hiyo.

Mohammed Dewji ni afisa mkuu mtendaji wa kampuni ya METL iliyoanzishwa na baba yake miaka ya 1970.

METL ina viwanda vya kutengeneza nguo na bidhaa nyingine za matumizi ya binadamu vikiwamo vyakula, sabuni na vinywaji. Pia ina mapato yanayozidi Dola 1.4 milioni za Marekani (Sh2.5 trilioni) kwa mwaka.

Katika kampuni hiyo, ambayo imekuwa na ushindani dhidi ya kampuni kubwa nyingine kama Said Salim Bakhresa, Dewji anamiliki asilimia 75 ya hisa zote.

Kwa mujibu wa tovuti yake, METL inaendesha shughuli za uagizaji na usafirishaji bidhaa kutoka na kwenda nje, uzalishaji unaohusisha nguo, vinywaji na vyakula, usagaji nafaka, nishati na petroli na utengenezaji baiskeli.

Pia inahusika na huduma za simu, fedha, kilimo na pia ina kitengo cha kontena kwenye Bandari ya Dar es Salaam.

METL ina shughuli zake katika nchi sita barani Afrika na ina malengo ya kujipanua zaidi katika maeneo zaidi.

Dewji ni mtanzania pekee aliyesaini mkataba mwaka 2016 wa kutoa kwa wahitaji nusu ya mali yake.

Mo Dewji Foundation ndio asasi ambayo aliianzisha ili kutekeleza nia yake hiyo na kazi yake kubwa ni kusaidia watanzania wasiojiweza kwa upande wa afya,elimu na maendeleo jamii.

Dewji pia ni mpenzi wa michezo na amewekeza katika klabu ya mpira ya Simba ya Tanzania.

Chanzo BBC.