Uturuki kuidhamini Zanzibar katika sekta ya Elimu

Serikali ya Uturuki imesema ipo tayari kuunga mkono  Nchi za Afrika ikiwemo Zanzibar katika Sekta ya Elimu ili kuziwezesha Nchi hizo kuendelea kuzalisha wataalamu wa fani mbali mbali katika nchi.

Akizungumza katika sherehe za kuanza mwaka mpya wa masomo 2019 katika skuli ya sekondari ya maarifu Wilaya ya kati Unguja, Balozi wa Uturuki nchini Tanzania Ali Davutaglu  amesema wapo tayari kusaidia sekta ya elimu kwa ngazi mbalimbali ikiwemo Elimu ya Masomo ya Sayansi.

Amesema mbali na kuanzisha skuli Zanzibar pia wamekusudia kuanzisha skuli nyengi Tanzania ili kurahisisha upatikanaji wa Elimu kwa wanafunzi jambo ambalo litaimarisha mashirikiano na uhusiano mzuri walionao kwa mda mrefu.

 akizungumza kwa Niaba ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya amali ,MKUU wa Mkoa wa Kusini Unguja, Hassan Khatib amesema serikali ya Zanzibar itaendelea kuthamini juhudi ya wahisani wa maendeleo katika kuimarisha sekta ya elimu Nchini.

Amesema wapo tayari kutoa ardhi kwa taasisi ya kimataifa ya Maarif kwa ajili ya kujenga skuli mpya ya Elimu ya Msingi pamoja na kujenga Chuo kikuu ambacho kitawawezesha wanafunzi kujifunza katika Nchi yao.

Ni jambo jema kuona wananchi wanajifunza fani mbalimbali katika Nchi yao jambo ambalo litawapunguzia gharama za masomo wanafunzi wenye kipato cha chini.

Aidha ametoa wito kwa wanafunzi wa skuli hiyo kusoma kwa bidiii pamoja na kuyapa umuhimu masomo ya sayansi ili kuendana na ulimwengu wa sayansi na teknolojia.

Taasisi hiyo ya Maarif ilianzishwa na bunge la Uturuki Juni 2016 kwa ajili ya kusaidia sekta ya elimu katika nchi mbali mbali duniani na ina vituo vya kutolea elimu zaidi ya 200 katika nchi 33 duniani kote.    

Na;Fat-hiya Shehe Zanzibar24.