Tundu Lissu, Mbunge wa Singida Mashariki amebainisha hayo katika taarifa yake aliyoitoa akiwa nchini Ubelgiji na kueleza kuwa kitendo hicho kilifanyika kabla hata ya Spika Ndugai kuombwa na kutoa mwongozo kuhusu mshahara wake.

Amesema uamuzi wa kufutiwa mshahara na posho za kibunge ambazo kila Mbunge hulipwa, awe anaumwa au mzima, awe amehudhuria vikao vya Bunge au la, ni uthibitisho mwingine wa ukiukaji wa Katiba, Sheria na taratibu.

“Ninaadhibiwa na tunaadhibiwa sio kwa sababu sisi ni wasaliti wa nchi yetu; bali ni kwa sababu ya kukataa kunyamaza na kufumba macho wakati maslahi halisi ya nchi yetu na wananchi wetu yanahujumiwa” Ameeleza Tundu Lissu.

Aidha, amelaani na kuita ni uamuzi haramu kwa mujibu wa Katiba ya nchi yetu, Sheria ya Uendeshaji wa Bunge na Kanuni za Kudumu za Bunge letu na pia haujazingatia misingi ya haki katika kufanya maamuzi yanayoathiri haki na maslahi yake.

Mapema mwezi uliopita Spika Job Ndugai aliobwa na kutoa mwongozo wa kusitisha mshahara na posho za Kibunge za Tundu Lissu kwa kusema kuwa hajahudhuria vikao vya Bunge bila ya ruhusa yake.